Mamlaka ya afya nchini China inajaribu kila njia kuudhibiti mlipuko wa virusi vya Corona ambavyo vimesambaa kote duniani tangu kuripotiwa katika mji wa katikati mwa China wa Wuhan zaidi ya mwezi mmoja uliopita kulingana na gazeti la South China Morning post.
Wakati huohuo , maafisa wanakabiliana na uvumi na habari ambazo hazijathibitishwa kuhusu mlipuko huo.
Haya hapa maswali yanayoulizwa.
1.Je virusi hivi vinaweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwengine?
Mtaalam wa ugonjwa wa Sars nchini China, Zhong Nanshan, alithibitisha wiki iliopita kwamba usambazaji wa virusi hivyo kutoka mtu mmoja hadi mwengine unaweza kufanyika, baada tume ya afya mjini Wuhan kusema hapo awali kwamba hakuna thibitisho la usambazaji wa virusi hivyo kutoka kwa mtu mmoja hadi mwengine.
Thibitisho kwamba ugonjwa huo unaweza kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja hadi mwengine limeungwa mkono na tafiti za kimatibabu ikiwemo moja iliochapishwa katika jarida la afya duniani la Lancet siku ya Ijumaa na wanasayansi kutoka chuo kikuu cha Hong Kong na maabara ya magonjwa yanayochipuka nchini humo.
Hatahivyo wataalam wanajaribu kubaini jinsi ugonjwa huo unavyoweza kusambazwa kati ya wanadamu kwa kupitia hewa.
Watu wanaosambaziwa kwa wingi ni wale walio na umri kati ya miaka 40 na 60 , wamesema maafisa wa afya nchini China.
Hatahivyo visa vipya vya ugonjwa huo vilivyothibitishwa vinahusisha msichana wa miaka miwili katika mkoa wa Guangxi na mwengine wa miezi tisa mjini Beijing, ikibaini kwamba watoto wadogo na wale wachanga pia wanaweza kuambukizwa.
Ni kweli virusi hivyo vinaweza kusambazwa miongoni mwa wanadamu.
2. Je kuna tiba yoyote ya ugonjwa huo iliothibitishwa?
Wanasayansi hawajapata tiba sahihi ya ugonjwa huo uliobainika hivi karibuni, ambao unaweza kusabababisha dalili nyingi miongoni mwa wagonjwa,ikiwemo kuharisha.
Vifo vingi kufikia sasa vimewakumba watu wenye magonjwa mengine kama vile kisukari , lakini mwathiriwa mwenye umri mdogo kabisa alikuwa mwanamume mwenye umri wa miaka 36 kutoka mkoa wa Hubei.
Tume ya afya mjini Beijing awali ilikuwa imesema kwamba itatumia dawa za kukabiliana na virusi vya ukimwi kama mojawapo ya tiba zake za virusi hivyo vya Corona.
Afisa mmoja anayefanya kazi na taasisi ya kitaifa ya afya wiki iliopita alisema kwamba shirika hilo lilikuwa linatengeneza chanjo ya virusi vya Corona ambayo huenda ikaanza kufanyiwa majaribio miongoni mwa wanadamu katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Wakati huohuo wanasayansi wa China na wenzao wa Marekani katika taasisi ya matibabu ya Beylor ilio mjini Houston, Texas, Chuo kikuu cha Texas na kile cha Fudan mjini Shanghai pia ziko katika awamu ya kwanza kutengeneza chanjo tofauti.
3. Je dawa za kitamaduni kama vile banlangen vina athari yoyote kwa virusi vya Corona?
Machapisho ya mitandao ya kijamii yamesema kwamba tiba za kiasili kama vile kugogomoa maji ya chumvi na kula karafuu iliochanganywa na vitunguu thumu kunaweza kutibu virusi hivyo.
Hatahivyo tume ya kitaifa ya afya wiki iliopita ilipinga uvumi kwamba unywaji wa mchanganyiko wa siki na dawa ya kitamaduni ya Wachina Banlangen kunaweza kutibu homa ya mapafu inayosababishwa na virusi hivyo.
Zhang Hua ambaye ni daktari wa magonjwa ya mapafu katika hopsitali ya Hepingli mjini Beijing, alinukuliwa akisema kwamba banlangen inaweza kutibu homa ya kawaida , lakini sio virusi vya Corona.
4. Je kuziba pua kunaweza kunilinda dhidi ya virusi hivyo?
Kujiziba pua kumekuwa kitu cha kawaida nchini China na Hong Kong baada ya visa vya ugonjwa wa virusi vya Corona kuongezeka katika kipindi cha wiki moja iliopita.
Huku idadi ya barakoa zinazotumika kujiziba pua zikiisha katika maduka mbali na mitandaoni kote nchini humo, watengenezaji wake wameshindwa kukabiliana na mahitaji yake.
Vifaa hivyo vinaweza kumsaidia anayevitumia kujiziba pua kutosambaza virusi hivyo kupitia mdomo na pua. Lakini uwepo wa mwanya kati ya anayevaa na kifaa hicho ni thibitisho kwamba kuna hatari kubwa ya kupata ugonjwa huo.
Wataalam wa kimataibabu ikiwemo shirika la afya duniani WHO wamependekeza hatua nyengine za kujilinda kama vile kuosha mikono mara kwa mara , kuziba mdomo wakati unapokohoa, kupiga chafya na kuzuia ulaji wa bidhaa za nyama ambazo hazijaiva.
5. Je uchunguzi wa viwango vya joto vya wasafiri katika maeneo kama vile viwanja vya ndege na vituo vya treni kunazuia kuenea kwa virusi hivyo hadi mataifa mengine?
Imethibitishwa kwamba wagonjwa wa virusi hivyo wanaweza kutoonyesha dalili za ugonjwa huo aina ya Pneumonia , lakini bado wanaweza kusambaza ugonjwa huo bila ya wao kuonyesha dalili kwa kipindi cha siku 14 ama wiki mbili.
Kulingana na David Heymann ambaye ni daktari wa magonjwa ya zinaa katika chuo kikuu cha London kuhusu usafi na dawa za kitropikali, uchunguzi wa kiwango cha joto katika mipaka sio asilimia 100 kwa kuwa watu wanaweza kupita vipimo vya joto bila kuonyesha dalili zozote.
Kitu muhimu na mipaka ni kuwaelezea watu mahala pa kwenda iwapo vipimo vya vya joto vipo juu, uchungu kooni ama kupumua kwa matatizo... mbali na kuimarisha mifumo ya kubaini ugonjwa huo hospitalini, katika kliniki na maeneo mengine nchini ili iwe rahisi kukabiliana na visa hivyo iwapo vitatokea, alisema Heymann.
Wiki iliopita , mwanamke kutoka Wuhan aliyekuwa na dalili za vipimo vya juu vya joto alipita vituo vya ukaguzi katika uwanja wa ndege nchini Ufaransa kwa kutumia dawa zilizoshukisha vipimo vyake vya joto.
Baadaye alitafutwa na ubalozi wa China nchini Ufaransa. Kutokana na hilo, ubalozi wa China umewataka raia wanaosafiri ughaibuni kuheshimu ukaguzi wa kiafya unaoendelea.
Virusi hivyo vimeshinikiza baadhi ya viwanja vya ndege duniani kuanzisha ukaguzi na hatua za haraka kwa wasafiri wanaotoka mji wa Wuhan na China.
6.Je imethibitshwa kwamba virusi hivyo vinatoka kutoka kwa wanyama wa mwituni katika soko la samaki mjini Wuhan?
Tume ya kitaifa ya afya nchini China ilisema siku ya Jumamosi kwamba sampuli 33 zilizochukuliwa kutoka katika soko hilo la Huanan mjini Wuhan vilithibitisha kuwepo kwa virusi hivyo.
Virusi hivyo hususan vilipatikana katika vibanda vya kuuza nyama , ambavyo vinauza wanyama wa mwituni.
Wataalam hawajabaini ni spishi gani ya wanyama walioasababisha maambukizi kwa binadamu , lakini tafiti mbili zinasema kwamba kuna uwezekano mkubwa kwamba vinatoka kutoka kwa popo ambao ndio chanzo cha virusi hivyo.
Hatahivyo , ripoti iliochapishwa katika jarida la Lancet siku ya Ijumaa inatoa changamoto ya maoni yanayolaumu mlipuko huo kutoka kwa soko hilo la vyakula vya baharini.
Ripoti hiyo inanukuu utafiti unaoonyesha kwamba wagonjwa 13 kati ya 41 hawakuwa na uhusiano na soko hilo la vyakula vya baharini.