Serikali ya Kenya imesema kwamba haitawarudisha nyumbani wanafunzi 75 wa Kenya walio mjini Wuhan China kufuatia mlipuko wa virusi vya Corona kulingana na gazeti la Nation nchini Kenya.
Wizara ya maswala ya kigeni nchini Kenya iliambia mkutano na wanahabari kwamba wanafunzi hao wapo salama pale walipo.
Imesema kwamba China inaisaidia Kenya kwa kila njia kuwaweka salama huku serikali ikitazama njia mbadala za kuangazia maslahi ya wanafunzi hao.
- Ukweli kuhusu dhana potofu zinazohusishwa virusi vya Corona
- Serikali ya Tanzania yawasihi wanafunzi kutorudi China
Hatahivyo Wuhan ndio chimbuko la virusi hivyo , ambavyo vimewaua watu 636 na kuwaambukiza wengine 31,000 kufikia sasa kulingana na takwimu mpya za tume ya kitaifa ya afya nchini China.
Wengi wa waathiri walikuwa wakitoka China bara.
Hatahivyo Muungano wa wanafunzi wa Kenya mjini Wuhan , katika barua yao kwa afisi ya wizara ya kigeni , imetoa ombi la serikali kuingilia kati , ukisema kwamba umeanza kukosa ufadhili wa vitu mbalimbali pamoja na kwamba wanahisi kuteswa.
''Kufikia leo ubalozi umeshindwa kujibu barua yetu wala kuonyesha wasiwasi. Tumewachwa katika kiza, ilisema barua hiyo iliotiwa saini na maafisa wa Muungano wa wanafunzi hao mjini Wuhan''.ilisema barua hiyo.
''Ubaya ni kwamba kila siku inapopita, hali iliopo mjini Wuhan inazidi kuwa mbaya . Baadhi ya wanafunzi hawana chakula huku wengine wakiwa na msongo wa mawazo kutokana na hofu inayozunguka tatizo lote''.
Wadi ya Hospitali ya Mbagathi
Serikali imesema kwamba imeanza kuimarisha uwezo wake wa kuwatambua wanaougua ugonjwa huo mbali na kuwapatia mafunzo maafisa wa afya kuhusu jinsi ya kukabiliana na virusi hivyo.
Mbali na hilo , wizara ya afya imetenga wadi yenye vitanda 120 katika hospitali ya Mbagathi kama mojawapo ya mipango ya kukabiliana na virusi hivyo, iwapo vitasambaa hadi Kenya.
Waziri wa afya anayeondoka Sicily Kariuki alitangaza hilo siku ya Ijumaa , lakini pia akasema kwamba hakuna visa vya virusi hivyo vinavyotoka Wuhan ambavyo vimethibitishwa nchini Kenya.
Vituo vya kuwatenga waathiriwa ambavyo vitakuwa katika eneo jipya katika hospitali ya Mbagathi , vinaongeza vitanda vingine 60 ambavyo vimetengwa katika hospitali kuu ya Kenyatta
Bi Kariuki pia alitangaza kwamba Kenya itapokea vifaa siku ya Jumamosi huku ikiendelea kuimarisha maabara kupitia kuongeza vifaa muhimu vya kupima na kutmabua virusi hivyo.
Ukosefu wa vifaa vinavyohitajika , na maabara katika kipindi cha wiki kadhaa zilizopita kumeifanya kenya kutuma sampuli zake kwa Taasisi ya kitaifa kuhusu magonjwa yanayosambazwa kupitia hewa nchini Afrika Kusini.