Mamlaka nchini Kenya zimepiga marufuku shirika la kimataifa la afya Marie Stopes kutoa huduma zozote zinazohusu utoaji mimba.
Bodi ya madaktari nchini Kenya inasema ilifanya uamuzi huo baada kuchunguza malalamiko kuwa matangazo ya shirika hilo yalikuwa yanaunga mkono utoaji mimba.
Utoaji mimba ni haramu nchini Kenya na huruhusiwa tu ikiwa mwanamke yuko hatarini.
Marie Stopes inasema inahudumu kuambatana na sheria, kwa kutoa ushauri na huduma baada ya utoaji mimba.
Mkuu wa shirika la serikali linalohusika na kuidhinisha matangazo, Ezekiel Mutua alikaribisha marufuku hiyo na kuilaumu serikali ya zamani ya Marekani kwa kuvunja maadili na kuunga mkono mkono utoaji mimba.
Baadhi ya wakenya wanahofu marufuku hiyo itachangia kuibuka kwa utoaji mimba haramu.
Kwa nini marufuku ikatangazwa?
Barua iliyotumuwa kutoka kwa Bodi ya Madaktari ya Kenya kwa Marie Stopes siku ya Jumatano ilisema: "Marie Stopes inaamrishwa kusitisha mara moja utoaji huduma wa aina zozote zinazohusu utoaji mimba kwenye Jamhuri ya Kenya.
Marie Stopes pia iliamrishwa kutoa ripoti ya kila wiki ya huduma zote iliyotoa kwenye vituo vyake ndani ya siku 60.
Bodi hiyo ilisema ilichukua hatua hizi kutokana na malalamiko kutoka Ann Kioko meneja wa shirika lililounga mkno maisha la CitizenGo Africa, na Ezekiel Mutua afisa mkuu wa mtendaji tume ya kudhibiti filamu nchini Kenya
Alfred Mutua alisema matangazo ya Marie Stopes hayakuwa yameidhinishwa na bodi na yalichangia ionekane kuwa ilikuwa vyema kwa mwanamke kutoa mimba.
Mwezi Januari Rais wa Marekani Donald Trump alisitisha ufadhili wowote wa Marekani kwa shirika lolote liliounga mkono utoaji mimba.
Marie Stopes ni nini?
Marie Stopes International linajivunia kuwa shirika kubwa zaidi duniani linalotoa huduma na utoaji mimba ulio salama likiwa na wafanyakazi 12,000 kwenye nchi 37 duniani.
Baada ya kuanzishwa mwaka 1976 lilikua na kusambaa kutoka kliniki ya Marie Stopes mjini London.
Ndicho kituo wanachotembekea wanawake walio na mimba wasiyoitaka, kwa mujibu wa gazeti la Kenya la Nation.
Mkurugezni wa Marie Stopes nchini Kenya Dana Tilson, aliliambia gezati hilo kuwa huduma za utoaji mimba wanazotoa zinaambatana na katiba.
Marie Stopes imesema nini?
Katika taarifa Marie Stopes inasema haijakiuka sheria kwenye nchi yoyote ambapo inatoa huduma zake.
Iliongeza kuwa inaungwa mkono na Wakenya:
"Kampeni yetu ya hivi majuzi ya kupunguza idadi ya wanawake wanaokufa kutokana na utoaji mimba usio salama imepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa watu wa Kenya."
"Wakenya wengi wanawajua takriban mwanamke mmoja ambaye amepoteza maisha kutokana na utoaji mimba usio salama na wamekaribisha fursa ya kujadili suala hilo muhimu."