Namna ya kumsaidia mjamzito anayetapika


HALI ya kusikia kichefuchefu na hatimaye kutapika ni tatizo ambalo huwaathiri wanawake kati ya asilimia 50 hadi 80 wanaopata ujauzito duniani kote. Hali hii inaitwa morning sickness, yaani ugonjwa wa asubuhi. Unaitwa hivyo kwa sababu mara nyingi kichefuchefu husumbua zaidi asubuhi ingawa kinaweza kutokea mchana ama muda wowote.
Kichefuchefu kinatoka na nini? Wanawake wamekuwa wakisumbuliwa na tatizo hili kwa karne nyingi, lakini chanzo chake hakifahamiki vyema ingawa kumekuwepo na nadharia nyingi ambazo bado zinafanyiwa kazi.
Inadhaniwa kwamba tatizo hili husababishwa na mabadiliko ya kifizikia na kikemikali tumboni; kuongezeka kwa homoni na kuongezeka kwa hali ya mjamzito kusikia harufu mbaya.
Nadharia moja kuhusu chanzo cha tatizo hili ni ile inayoonesha kwamba linatokana na kuongezeka kwa homoni aina ya estrogen na progesterone, humfanya mwanamke kusikia harufu mbaya huku tindikali pia ikiwa imeongezeka tumboni.
Inaaminika pia kwamba hali ya uchovu na hisia nzito ama mawazo mengi ambayo mara nyingi humpata mjamzito, vinachangia pia tatizo hili. Nadharia kuhusu homoni ambazo huwa nyingi zaidi wakati wa ujauzito, ndizo zinazozungumzwa zaidi kusababisha kichefuchefu.
Homoni za Progesterone zina tabia ya kulainisha misuli ya mwili na hii hufanyika ili kupunguza maumivu ya uzazi kwa kusaidia misuli ya tumbo la uzazi kulainika. Vile vile homoni hizi huathiri pia baadhi ya misuli kama vile tumbo na utumbo mwembamba.
Homoni za progesterone hupunguza kasi ya mfumo mzima wa uyeyushaji wa chakula mwilini, hali ambayo husababisha tumbo pia lisifanye kazi ya kutoa uchafu tumboni haraka na hivyo kuongezeka kwa tindikali nyingi.
Nadharia nyingine ambayo pia hukubalika na wasomi ni kwamba tatizo la kichefuchefu husababishwa na kujirundika kwa kitu kiitwacho kwa kitaalamu, human chorionic gonadotopin (hCG) kwenye tumbo. hCG huanza kuzalishwa baada ya mwanamke kunasa mimba na huendelea kuongezeka hadi mimba inapofikisha wiki 12 ambapo kasi ya hCG huanza kupungua.
Kwa wanawake wengi ni kipindi hiki pia ambacho tatizo la kichefuchefu huanza kupungua pia. Kuna nadharia nyingine ambayo pia hutajwa na wajuzi wakisema kuwa kichefu chefu chanzo chake ni kupungua kwa sukari mwilini, hasa katika wiki za awali za ujauzito.
Pia kuna nadharia inayoonesha kwamba wanawake wenye kawaida ya kula vyakula vyenye mafuta mengi huathirika zaidi kulinganisha na wale wanaokula vyakula visivyokuwa na mafuta.
Hata hivyo, tatizo hili la ‘ugonjwa wa asubuhi’ si kitu kibaya kwani tafiti nyingi zinaonesha kwamba wanawake wengi wanaokumbwa na tatizo hili ni mara chache kuwa na matatizo ya mimba kuharibika (miscarriages).
Pia madaktari wengi wanaamini tatizo hili na dalili nzuri kwamba baada ya mwanamke kuzaa, kuta za tumbo la uzazi hujengeka vyema.
Ingawa baada ya wiki 12 tatizo hili mara nyingi huanza kupungua, lakini baadhi ya akina mama huendelea kutapika hadi siku ya kujifungua. Hali hii ikitokea mara nyingi huathiri shughuli za mama za kila siku katika maisha yake pamoja na familia yake. Kutapika kunaweza kuathiri mtoto tumboni?
Si mtoto tu, hata mama yake kama atatapika sana na kuishiwa maji na chakula mwilini, vitu ambavyo ni muhimu kwake na kwa afya ya mtoto. Katika hali kama hiyo mjamzito anaweza kupungua uzito kwa kasi, jambo ambalo halishauriwi.
Tatizo la kutapika mjamzito huchukuliwa kama la kawaida lakini kuna wakati huwa baya zaidi na huitwa kwa kitaalamu hyperemesis gravidarium (HG). Wawanake ambao hukumbwa na tatizo hili mara nyingi ni wachache, yaani kati ya asilimia 0.5 hadi mbili ya wajawazito wote.
Kama HG haitatibiwa inaweza kuhatarisha maisha ya mama na mtoto tumboni. Tatizo hili la HG hutokea pale mjamzito anaposikia kichefu kuliko kawaida na kutapika kunakozidi mipaka. Inaweza kusababisha mjamzito kuishiwa maji, kupungua uzito na kupoteza virutubisho vingi vya mwili.
Mama anapofikia hali hii inabidi amuone daktari haraka kwa uangalizi wa karibu. Dalili za HG ni pamoja na kichefuchefu kinachokithiri, kutapika kunakoendelea (zaidi ya mara 3 au 4 kwa siku), kupungukiwa na maji mwilini na kupungua kwa virutubisho vya mwili kutokana na kupungua kwa maji.
Dalili zingine ni kupunguka uzito ama kushindwa kuongezeka uzito, mapigo ya moyo kuongezeka, ngozi kuonekana kavu na kichwa kuuma, na wakati mwingine mjamzito anaweza kupata hali kama ya kuchanganyikiwa. Ili kujua kama mjamzito kapungukiwa maji la kufanya ni pamoja na kuvuta ngozi yake ambapo hurudi taratibu.
Lingine ni ngozi inaonekana ikiwa kavu, kupungukiwa machozi ama mate, ulimi kukauka, kuchanganyikiwa ama, mawazo mengi ama hasira, kupungukiwa na mkojo (kukaa muda mrefu bila kukojoa ama kukojoa mkojo ‘kiduchu’) na mkojo kuwa wa rangi ya ugoro iliyokolea.
Kama mjamzito ana dalili hizo anatakiwa kumuona daktari haraka. Kuna hatua ambazo daktari atazichukua ili kusaidia tatizo lake na inasisitizwa kwamba hali ikifikia hivyo si tatizo la kupuuzia.
Namna ya kukabiliana na kichefuchefu Hatua za awali kwa mjamzito anayesumbuliwa na kichefu chefu ni pamoja na kwamba, kwa vile katika miezi mitatu ya mwanzo hadi minne, pua zake ni rahisi kusikia harufu, inashauriwa akae katika chumba chenye hewa ya kutosha ambacho hakisababishi hakikusanyi harufu kali kama vile mapishi ama sigara. Sambamba na hilo aepuke kukaa sehemu zenye harufu mbaya na inayokera pua.
Pili, aepuke kukaa eneo lenye joto kwa sababu joto linaaminika kuongeza kichefu chefu. Anashauriwa pia apendelee kula vitu vikavu, kama bisi, tambi, kaukau za chips na ikiwezekana afanye hivyo dakika 15 kabla ya kuamka kutoka kitandani asubuhi. Kwa hiyo ahakikishe vyakula vikavu haviko mbali na kitanda chake. Nne, ale chakula kidogo kidogo kila baada ya saa mbili ama tatu.
Tumbo linapobaki wazi kwa muda mrefu linaweza kuongeza hali ya kujisikia kichefuchefu. Ale chakula chenye protini ya kutosha na wanga (siyo mafuta) kwani hivyo vyote viwili husaidia kupigana na hali ya kichefuchefu. Pia chakula kisiwe na harufu kali ama kisiwe kimekaangwa sana. Vyakula chukuchuku vinafaa zaidi.
Tano, anyanyuke taratibu na asilale haraka haraka baada ya kula chakula na pia asiache kula bila sababu na hasa kula kile anachotamani. Katika hali ya kichefuchefu anashauriwa ajaribu kula hata kama si sehemu ya chakula ulichozea kila siku. Lingine ni kunywa maji nusu saa kabla chakula na nusu saa baada ya chakula.
Kwa lugha nyingine, asinywe maji pamoja na chakula. Ahakikishe unakunywa wastani wa glasi nane za maji kwa siku ili kuepuka hali ya kupungukiwa maji mwilini.
Kama harufu inamuudhi wakati wa kupika na yeye ndiye analazimika kupika, ajaribu kupikia sehemu yenye uwazi wa kutosha, madirisha makubwa ama hata nje ya nyumba. Kama inawezekana, atafute mtu mwingine amsaidie kutayarisha chakula.
Ajaribu pia kula chakula kilichopoa badala ya cha moto. Chakula kilichopoa kina harufu kidogo kulinganisha na cha moto. Pia inashauriwa kwamba chakula wakati huu kisiwe na chumvi nyingi. Harufu ya limao ama ndimu iliyokatwa inaweza kusaidia pia kupunguza kichefu chefu.
Anaweza pia kuweka limao kidogo kwenye chai yake au hata maji. Na mwisho mjamzito anayesumbuliwa na kichefuchefu apate muda mwingi wa kupumzika.
Kuongea mambo ya mimba na akina mama wengine wenye kujua tatizo lake kunaweza pia kusaidia hali ya kupunguza mgandamizo/ mawazo mazito kichwani, kwani kama ilivyoelezwa mwanzo, nadharia moja ambayo watu wanahisi kuwa inasababisha kichefuchefu ni hali hiyo ya mawazo mengi.
Vitu au dawa za kusaidia Tangawizi ni zao la asili ambalo mara nyingi linashauriwa katika kutibu kichefuchefu na kutapika kwa mwanamke mjamzito.
Baadhi ya tafiti zimeonesha kuwa tangawizi inasaidia sana kupunguza kasi ya kichefu chefu kwa wanawake wajawazito. Mgonjwa pia anaweza kutumia kidonge cha Diclectin: Dawa hii muungano wa vitamin B6 na dawa zinazozuia mzio (antihistamine) aina ya doxylamine.
Dawa hizi zimetengenezwa viwandani kwa ajili ya kuzuia kichefu chefu na kutapika. Dawa hizi zimekuwa zikitumiwa zaidi nchini Canada na wanawake wengi wamesema kwamba zinawasaidia.
Hata hivyo, baadhi ya wanawake wamedai kusikia hali ya kizunguzungu wanapotumia aina hii ya dawa. Kadhalika kuna dawa mbalimbali ambazo madaktari wanaweza kumpa mgonjwa ili kusaidia katika tatizo hili.
Kumuona daktari Mbali na kumuona daktari kutokana na kutapika sana hadi kuonesha dalili ya kuishiwa maji ama kupungua uzito, inapaswa kumuona daktari endapo tatizo la kutapika halikomi baada ya kujaribu mambo ambayo tumeyaorodhesha hapo juu.
Pili mjamzito amuone daktari kama anatapika damu ama vitu ambavyo vinafanana na mbegu za kahawa. Mgonjwa akifika hospitali, daktari anaweza kutaka kujua historia ya ugonjwa wake, hususan kuhusu ni mara ngapi kwa siku kichefuchefu hutokea na kama kinakutokea kila siku ama la.


Post a Comment

Previous Post Next Post