MWAKA 2015, Mariam John alijifungua salama mtoto wake wa
pili Elizabeth Peter (si majina yao halisi), huko mkoani Kigoma ambako ndipo
yalipo makazi yao.
Maendeleo ya afya ya Elizabeth yalikuwa yanaridhisha kila
walipohudhuria kliniki lakini miaka miwili baada ya kuzaliwa hali ilianza
kubadilika ghafla.
Mariam anasema siku moja alipokuwa akimnawisha sehemu ya
haja kubwa mtoto wake huyo, baada ya kumaliza kujisaidia alishangaa kugusa
kinyama ambacho kilijitokeza kwa nje.
Daktari Bingwa wa
Upasuaji wa watoto Muhimbili, Zaituni
Bokhary anasema Elizabeth alipata tatizo linalojulikana kitaalamu Rectal
Prolapse.
“Hii ni hali ambayo sehemu ya utumbo mkubwa iitwayo ‘rectum’
hutoka nje ya mwili katika njia ya haja kubwa. Hakuna sababu maalumu ambayo
wataalamu tunaweza kusema moja kwa moja, kwamba tatizo limesababishwa ama na
bakteria au wadudu. Lakini kuna viashiria au visababishi kadhaa ambavyo
vinahusishwa kusababisha tatizo hilo kutokea” .
Visababishi
Hali hiyo inaweza kusababishwa na kuharisha muda mrefu hali
ambayo huchangia mtoto kupungua uzito na kukonda mwili. Hii ni sababu kuu,
kuharisha muda mrefu husababisha mtoto kukonda hadi ile misuli ya haja kubwa
hushindwa kukaza vizuri kama inavyotakiwa hali hiyo huifanya ile ‘rectum’
kutoka nje
Kiashiria kingine cha awali ambacho mzazi anaweza kukiona
iwapo mtoto anakabiliwa na tatizo hilo ni kupata viotea (vinyama) ambavyo
hutoka katika njia ya haja kubwa. Vinyama hivyo hutoka nje ya mwili katika
sehemu ya haja kubwa. Wakati mwingine tatizo huweza kujitokeza iwapo kuna
maambukizi katika utumbo mkubwa
Iwapo mtoto aliwahi kufanyiwa upasuaji wa utumbo mkubwa,
inaweza kusababisha akapatwa tatizo hilo kwa namna moja au nyingine.
Lakini wengine wanapata tatizo hili, ikiwa wamezaliwa na
hawana chembe chembe maalumu ambazo kazi yake kuu ni kusukuma choo nje ya
mwili, sasa kwa kuwa hajazaliwa na chembe chembe hizo mtoto huyo anaweza utumbo
wake ukatoka nje kwa sababu ya kutumia nguvu kusukuma choo
Hatua za tatizo
Daktari huyo anasema ugonjwa huo hupitia hatua kuu nne na
kwamba iwapo mzazi atawahi kumfikisha mwanawe hospitali matibabu yanaweza kufanyika bila kutumia njia ya upasuaji ila endapo atacheleweshwa kupatiwa matibabu kwa dalili za awali matibabu yatahiji njia ya upasuaji.
HATUA YA KWANZA
Katika hatua ya kwanza mzazi au mlezi ataona ule utumbo
unatoka na kurudi ndani wenyewe, sasa anapomleta hospitali mtoto anamfanyia
uchunguzi kujua nini kinasababisha hali hiyo, atatibiwa kwa kutumia dawa maalumu
na wala hatahitaji kufanyiwa upasuaji wowote
HATUA YA PILI
Anataja hatua ya pili ya tatizo kuwa utumbo unapotoka nje
hushindwa kurudi ndani bila kusaidiwa kuurudisha.
HATUA YA TATU
Kwa maelezo ya kidaktari “hatua ya tatu huashiria kwamba
tatizo linazidi kuwa kubwa na kwamba utumbo wa mtoto huweza kujitokeza nje hata
kama hakujisaidia.” Inapofikia hatua hii matibabu hufanyika kwa njia ya
upasuaji.
JINSI YA KUMKINGA
MTOTO
watoto wengi ni rahisi kupatwa na hali hiyo hasa wale
wanaoishi katika mazingira machafu.
Inaaminika kwamba tatizo
la kuharisha maana yake amekula vitu vichafu, watoto wanapocheza hushika vitu vingi, na
wengi hupenda kuweka vidole mdomoni.
mazingira yanapokuwa
machafu mtoto anakuwa kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi, ni vema
mazingira yakasafishwa kila wakati yawe rafiki kwa watoto ili kuwaepusha
Pindi tu uonapo dalili zilizotajwa hapo juu ni vema kwenda
kwenye kituo cha afya kupata matibabu zaidi.
Tags:
MAGONJWA YA WATOTO