Mwanamke mmoja raia wa Bangladesh amejifungua mapacha wawili karibu mwezi mmoja baada ya kujifungua mtoto njiti, Daktari wake ameiambia BBC
Arifa Sultana,20, alijifungua mtoto wa kiume mwishoni mwa mwezi Februari, lakini siku 26 baadae alikimbizwa tena hospitalini baada ya kupata maumivu ya tumbo.
Madaktari waligundua kuwa bado ni mja mzito wa watoto mapacha katika mji wake mwingine wa mimba, kisha alifanyiwa upasuaji wa dharura.
Watoto wake wamezaliwa wakiwa na afya njema kisha wakaruhusiwa kwa kuwa hawakuwa na tatizo lolote.
'Tulishtuka'
Bi Sultana, kutoka katika kijiji kimoja, alijifungua mtoto wake wa kwanza katika Hospitali ya chuo cha Khulna katika wilaya ya Khulna.
Siku 26 baadae, alilalamika kuumwa tumbo akakimbizwa kwenye hospitali nyingine katika wilaya ya Jessore tarehe 21 mwezi Machi, Daktari Sheila Poddar, daktari wa magonjwa ya wakina mama aliyemfanyia upasuaji aliiambia BBC.
''Mgonjwa alipofika tulifanya kipimo cha Ultrasound na kugundua kuwa kulikua na mapacha tumboni mwake,''Dokta Sheila Poddar alieleza.
''Tulishtuka sana na kushangaa.Sikuwahi kukutana na kitu kama hiki .''
Haijijulikana kwa nini aliamua kwenda kwenye hospitali tofauti.
Kwa mujibu wa Poddar, Bi Sultana na mumewe ni ''fukara'' na hakuwahi kufanya ultrasound kabla'', kabla ya kujifungua mtoto wake wa kwanza.
Hakua akijua kuwa alikua na watoto wengine,'' Alisema Dokta Poddar.''Tulifanya upasuaji na alipata watoto wawili pacha wakiume na wakike.''
Mtaalamu wa magonjwa ya wanawake nchini Singapore anasema kitaalamu hali ya mtu kuwa na chupa mbili za uzazi ''si jambo la ajabu kama watu wanavyofikiri''.
''Ikiwa utakwenda kwenye vipimo kabla, ni wazi kabisa utaziona chupa mbili.Lakini ni wazi anatoka eneo la vijijini ambapo huenda hakuna huduma ya Ultrasound.'' Alieleza daktari Christopher, mtaalamu wa magonjwa ya wakina mama.
''Mayai matatu yalizalishwa na kupevushwa kwa wakati mmoja wakati wa kutungwa mimba ambayo ilisababisha kupata viumbe vitatu.''
Bi Sultana anasema ana furaha na watoto wake watatu lakini ana changamoto kuhusu malezi yao kwa sababu za kiuchumi, kwa mujibu,Shirika la habari la AFP limeeleza.
Mume wake hupata kiasi cha chini ya dola 95 za Marekani kama ujira wake kwa mwezi, lakini anasema atajitahidi kumudu gharama.
''Ni muujiza kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwamba watoto wangu wote wana afya njema.Nitajitahidi kuwapa furaha.