Mtuhumiwa wa mauaji ya watu 50 kwenye mashambulizi ya misikiti miwili mwezi uliopita nchini New Zealand ameamriwa kupimwa akili.
Kwa mujimu wa Jaji wa Mahakama Kuu, Cameron Mander, mtuhumiwa huyo atapimwa na madaktari bingwa wa afya ya akili ili kuamua iwapo anaweza kuendelea na kesi hiyo ama ni mgonjwa wa akili.
Mtuhumiwa huyo anakabiliwa na mashtaka 50 ya mauaji na mashtaka 39 ya kujaribu kuua.
Raia wa Australia Brenton Tarrant, 28, alihudhuria kesi hiyo kwa njia ya simu ya mtandao kutokea gerezani. Chumba cha mahakama kilijaa ndugu za watu ambao waliuawa kwenye mashambulizi hayo.
Mshatakiwa huyo hakutakiwa kusema chochote.
Mashambulio hayo ni makubwa zaidi katika historia ya taifa la New Zealand.
Waziri Mkuu wa nchi hiyo aliiita siku ya mashambulizi kuwa ni moja ya siku za kiza zaidi kwa New Zealand.
Pia ameazimia kupiga marufuku umiliki kwa raia wa silaha zote za sampuli ya kivita.
Nini kilitokea mahakamani?
Jaji Mander ameamuru mtuhumiwa achunguzwa afya yake ya akili mara mbili ili ibainike yupo katika hali gani.
Mtuhumiwa huyo alikuwa kimya akisikiliza kwa makini kilichokuwa kikiendelea mahakamani. Hakuongea kitu.
Aliweza kuwaona jaji na wanasheria tu, kamera haikuelekezwa walipo wasikilizaji wa kesi.
Jaji ameamuru aendelee kusalia rumande mpaka pale kesi yake itakapotajwa tena Juni 14.
Omar Nabi alimpoteza baba yake kwenye shambulio la msikiti wa Al Noor. Akiongea na waandishi nje ya mahakama amesema "hatutaki kumuua. Tunataka ateseke tu."
"Tunataka aadhibiwe, unajua, adhabu kali ya jinai ya kuua wato 50 na kujeruhi sijui wangapi."
Tofazzal Alam ambaye alinusurika kwenye msikiti wa Linwood pia alipata wasaa wa kuzungumza na waandishi nje ya mahakama.
"Nimepoteza marafiki 50 ambao nilikuwa nikiwaona msikitini kila Ijumaa. Na wakati wa shambulio, sikuiona sura yake. Nataka nimuone anajisiaje baada ya kuua watu 50. Ndio maana nipo hapa leo."
Mashambulio hayo yalitokeaje?
Mshukiwa huyo alikamatwa Machi 15 kutokana na uhusika wake kwenye mashambulizi hayo kwenye misikiti ya Al Noor mosque na Linwood yote iliyopo mjini Christchurch.
Anadaiwa kwanza kuushambulia msikiti wa Al Noor, ambapo aliegesha gari yake karibu na msikiti huo a kuingia kupitia lango la mbele na kuwamiminia risasi wanaume, wanawake na watoto kwa dakika tano.
Shambulio hilo alilirusha mbashara kwenye mitandao ya kijamii kupitia kamera aliyoivaa kichwani, na pia alijionesha uso wake wakati akiendele na shambulizi.
Baada ya hapo mshukiwa huyo anadaiwa kutimka na gari yake mpaka kwenye msikiti wa Linwood ambapo aliendeleza mashambulizi yake.
Misikiti hiyo ipo umbali wa kilomita 5.
Bwana huyo alikuwa amejihami na bunduki ya kivita aina ya AR-15, ambayo aliiboresha ili kubeba risasi nyingi zaidi ya kawaida.
Kwa sasa anashikiliwa kwenye gereza la Paremoremo, ambapo amewekwa kwenye seli ya peke yake.
Nchi ya New Zealand imepokea vipi tukio hilo?
Chini ya wiki moja toka tukio hilo litokee, Bi Arden alitangaza marufuku ya umiliki wa raia kwa silaha za kivita.
Ameahidi sheria hiyo mpa itaanza kutumika kuanzia Aprili 11.
Raia wengi wa taifa hilo kwa sasa bado wangali katika bumbuwazi juu ya namna gani mauaji hayo yamefanyika.
Zaidi ya wakaazi 20,000 walijitokeza kuomboleza kwa pamoja mashambulizi hayo kwa kuyakumbuka maisha ya wahanga wote 50 waliouawa.
Waliouawa ni watu wenye asili na kutokea nchi mbali mbali duniani, na mdogo kabisa alikuwa mtoto wa miaka 3.