Maelfu ya raia wa Tanzania jijini Dar es Saalam, wanaendelea kuomboleza kifo cha Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group Tanzania, na mhamasishaji mkubwa wa vijana katika matumizi ya vipaji na fursa, Rugemalila Mutahaba maarufu kama Bosi Ruge.
Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa na baadhi ya viongozi wengine wa kitaifa akiwemo Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Akson wamefika nyumbani kwa Marehemu na kumuelezea wasifu wake. Mipango ya kurejesha mwili wa marehemu kutoka nchini Afrika kusini alikopelekwa kwa matibabu inafanyikaHuzuni
Msongamano wa waombolezaji ni mkubwa waliofika nyumbani kwa marehemu wakiwemo viongozi mbalimbali na watu maarufu. Waziri mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa anamuelezea Ruge kuwa Kielelezo cha tafsiri ya kiongozi kijana mwenye fikra na maono chanya kusaidia wengine na nchi kwa ujumla
"Vijana hasa katika eneo hili la sanaa, walikuwa na kiongozi ambaye alikuwa tayari kuwaongoza na kuwasaidia, nayasema haya kuonyesha namna ambavyo tulivyopoteza mwenzetu, lakini kubwa ndani ya serikali kuisaidia utafasiri 'filosofia" ya uzalendo na fursa kwa watanzania.''
Kwa vijana wengi kifo cha Ruge ni taa iliyozizima katikati yam situ mnene kwenye giza nene, wengi wao hawaoni kesho yao inafafanaje.
Rehema Jonas ni mmoja wa vijana waliofanikiwa kupitia programu za vijana katika kujenga uwezo wao , kujitambua na kuchukua hatua iitwayo 'fursa' amesema ''sisi ni vijana ambao tuko mtaani tunavipaji tu vya kuweza kufanya jambo Fulani, kwa hiyo mimi maisha yangu yote nimekuwa nikiishi kwa kauli ya Ruge. Tangu ameanza kuumwa nilianza kuona giza mbele, alikuwa ni zaidi ya Bosi, mshauri na rafiki".
Buriani Ruge Mutahaba
Msanii maarufu na wa siku nyingi wa muziki wa kizazi kipya ambaye amelelewa na kukuzwa kimuziki na Ruge kupitia kituo chake cha sanaa cha Tanzania House of Talents (THT), Lameck Ditto anakiri kuwepo kwa hofu ya muelekeo wa muziki huo. " Kwanza ni mshituko na hiyo hofu inakuja kwa sababu alikuwa mtu aliyekuwa anaweka mawazo yake yote katika kazi, lakini ametufundisha ni kuhakikisha tunajitahidi kwa kadiri tunavyoweza kukabiliana na changamoto tunazopitia''.
Kwa upande wake Joseph Kusaga, Mkurugenzi mwenza wa kampuni ya Clouds Media Group(CMG) inayomiliki vituo maarufu vya Televisheni na Radio vya Clouds, Joseph Kusaga, ametoa matumaini kwa vijana akisema kuwa vijana waliopita kwenye mikono yake watakuja kuendeleza yale mazuri aliyoyafanya.