Mama wa mtoto aliye raia wa Yemeni amezuiwa kumuona kijana wake aliye karibu kuaga dunia kutokana na sheria ya kuwazuia wageni kutoka nchini mwake, familia imeeleza.
Mtoto Abdullah Hassan alizaliwa na maradhi ya ubongo ambapo madaktari walisema hataweza kuishi.
Ndugu wanasema mama yake anataka kumuona kwa mara ya mwisho kabla ya kuondoa mashine ya kumsaidia kupumua.
Baba yake anasema mama wa Abdullah hawezi kwenda nchini Marekani kutokana na marufuku iliyowekwa na utawala wa Trump.
Abdullah na Baba yake ni raia wa Marekani, familia imeeleza.
''Anachotamani ni kushika mkono wa mtoto wake kwa mara ya mwisho'', Baba wa mtoto Ali Hassan aliliambia gazeti la San Francisco Chronicle.
Amesema mtoto atapoteza maisha kama atapelewa Misri, ambako mama yake anaishi kwa sasa.
Mke wa Hassan, Shaima Swileh, anatafuta ruhusa kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Marekani ili aweze kuingia nchini humo haraka
Marufuku kuingia Marekani
Muda mfupi baada ya kuingia madarakani, Rais wa Marekani, Donald Trump aliweka marufuku ya kuingia Marekani akizigusa nchi kadhaa hasa za kiislamu.
Marufuku hiyo imewekwa kwa raia wa nchi ya Iran, Korea Kaskazini,Venezuela,Libya,Somalia,Syria na Yemen.
Hatua hiyo yaelezwa kuwa ni 'ukatili'
Saad Sweilem, kutoka Baraza la kiislamu la nchini Marekani, amesema kumzuia mama wa mtoto Abdullah ni ''ukatili wa hali ya juu''
Baba wa Abdullah alizaliwa California, lakini amekuwa ana ndugu zake na familia iliko asili yao nchini Yemen.
Hassan alikutana na mkewe nchini Yemen, na wawili hao walipata watoto saba nchini humo.
Abdullah alikutwa na maradhi ya ubongo kwa kitaalamu hypomyelination ambayo yameathiri uwezo wake wa kupumua.
Alipokua na umri wa miezi minane,familia iliondoka Yemen kuelekea Cairo, kukwepa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Takriban miezi mitatu illiyopita, Bwana Hassan alimpeleka mtoto nchini Marekani kwa ajili ya kupata matibabu, akiwa na matarajio kuwa mke wake ataungana nao baadae.
Lakini baada ya madaktari mjini Oakland, California, kumjulisha kuwa hali ya mtoto ni mbaya sana, familia ilianza kushughulikia vibali vya kumuwezesha mama wa mtoto kufika Marekani.
Wamesema walipokea barua ya kukataliwa ombi lao kutoka wizara ya mambo ya ndani, wakirejea marufuku iliyowekwa na Trump.
Afisa kutoka idara hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina alikataa kujadili kuhusu suala hilo.