'microcephaly' katika pwani ya Kenya inavyowakumba watoto.

microcephaly
Kwa zaidi ya muongo mmoja baadhi ya familia katika kaunti ya Kilifi nchini Kenya wamekuwa wakijifungua watoto wenye hali isio ya kawaida.
Katika hali hiyo inayojulikana kama microcephaly ubongo wa mtoto haukuwi kama unavyohitajika kawaida na hivyobasi kusababisha hali ya mtoto kuwa na kichwa kidogo ikilinganishwa na watoto wengine umri wao.
Hatahivyo katika vijiji hivyo vya mashambani , jamii imekuwa ikiwatelekeza watoto wenye hali hiyo na sasa wamekuwa wakichukuliwa kama watu wenye laana na wanaosababisha majanga.
Kulingana na wakaazi wa vijiji hivyo, watoto wenye aina hiyo ya ulemavu wanaaminika kuzuia mvua kunyesha na hivyobasi kudaiwa kuwa chanzo cha baa la njaa katika vijiji maskini katika maeneo ya Bamba na Ganze.
Hivyobasi familia ambazo huwazaa watoto kama hawa hutakiwa kuwaua ama hata kulazimika kuhama vijiji hivyo ili kukwepa shutuma kutoka kwa wakaazi.
Familia moja kama hiyo ni ile ya mzee Nzai Menza ambaye anasema kuwa alilazimishwa kuondoka nyumbani kwao huko Ganze na kuhamia katika mji wa Mtwapa uliopo kaskazini mwa mji wa Mombasa baada ya mkewe kujifungua mtoto mwenye ulemavu huo.
microcephaly
''Nililazimishwa kuondoka kijijini kwa sababu hakuna mtu aliyetaka kujihusisha na mtoto huyu. Hata wazazi wangu walikuwa wakiniambia nimuue ama hata kumtupa msituni'' , anasema.
Menza ambaye ni baba ya watoto watatu waliozaliwa bila ulemavu huo, anasema kuwa ametafuta usaidizi kutoka kwa baadhi ya madaktari kuhusu hali hiyo bila mafanikio yoyote.
Hatahivyo mtoto huyo Leah ambaye ana miaka 14 lakini ana umbo la mtoto wa miaka minne amepata mahali anapoita nyumbani katika shule maalum ya Sahajanad ambapo amejiunga na mamia ya watoto walio na ulemavu.
Watoto wanaougua 'microcephaly' pwani ya Kenya watelekezwa
Kwake Leah, Shajanand ni shule ambayo anaweza kuchanganyika na watoto wenye ulemavu kama wake na kuweza kuishi bila kuhisi kwamba anabaguliwa na mtu yeyote yule.
Kulingana na mwalimu mkuu wa shule hiyo Patrick Mzungu, watu wanaamini kwamba watoto hawa wanaleta bahati mbaya sio tu kwa familia bali pia kwa jamii. Anasema kuwa baadhi ya watoto hao wamekuwa wakitumika katika matambiko kuwatakakasa watu wazee waliofariki na magonjwa ya zinaa.
microcephaly

Mazingira wanayoishi

Katika shule ya Sahajanand watoto hao wanaweza kutabasamu , wana udugu maalum na inaonyesha lengo lao la kutaka kuishi mbali na jamii ambayo imewakataa. Wengi ya watoto hao huletwa katika shule hiyo na wazazi ambao wanahofia maisha yao ama hata kuokolewa na utawala wa maeneo hayo.
Katika jamii ambayo inaamini tamaduni zilizopitwa na wakati na ushirikina, watoto hawa hawana fursa ya kuishi nje ya kuta ndefu za shule hii.
''Kuna mtoto ambaye tulimuokoa katika eneo la Baringo baada ya mvulana huyo kuangaziwa na vyombo vya habari kwamba alikuwa amefungwa kamba katika msitu ili afariki. Tulienda na vyombo vya habari kumuokoa mtoto huyo na sasa yuko hapa na ameimarika'' anasema bwana Mzungu.
Babake Leah ameisifu shule hiyo kwa kuimarisha hali ya mwanawe.
microcephaly

Microcephaly ni nini?

Ugonjwa huo wa kichwa kidogo unahusishwa sana na Virusi vya Zika.
Mnamo mwaka 2016 virusi vya Zika vilitangazwa kuwa janga la dharura ambalo limezua wasiwasi kimataifa.
Zika ilitajwa kuwa ugonjwa hatari katika kiwango kimoja na ugonjwa wa ebola.
Lakini kile kinachowashangaza wengi ni idadi kubwa ya watu walio na ulemavu huo katika eneo hilo la mashambani la pwani ya Kenya .
Baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wanaamini kwamba visa vya watu wa uhusiano wa karibu kujamiana huenda ndio chanzo cha ongezeko la watoto wanaozaliwa na Microcephaly.
Lakini kulingana na daktari Ahmed kalebi hali ni tofauti katika kaunti ya Kilifi.
''Kuna data inayoonyesha kwamba viwango vya microcephaly katika kaunti ya kilifi iko juu ikilinganishwa na maeneno mengine duniani na hata Kenya, na baadhi ya tafiti zinasema kuwa huenda ugonjwa huo
ukahusishwa na ugonjwa wa pepo punda.
Sidhani iwapo tumefanya utafiti wa kutosha , lakini wakati kulipokuwa na mlipuko wa Zika kuna data inayoonyesha kwamba watu wa pwani ya Kenya wana viwango vya juu zaidi vya watu wenye kinga dhidi ya Zika'', anaeleza daktari Ahmed Kalebi.
microcephaly
Wakati huohuo jukumu kuu la mwalimu mkuu Patrick Mzungu sasa ni kuhakikisha kuwa jamii yake inaelemishwa kuhusu hali hiyo, na pengine kuwashawishi kwamba huu ni ugonjwa kama mwengine wowote ule.
''Watoto hawa wana haki ya kuishi, hatukuenda kwa Mungu kumuuliza tuzaliwe na vichwa vidogo, hata wazazi hawakumuuuliza Mungu kuwapatia watoto wenye microcephaly, kwa hivyo tafadhilini sana hawa ni binadamu na ulemavu huu ni kama mwengine wowote ule tunaoishi nao''.
Shirika la afya duniani linasema kuwa kuna sababu nyingi za ugonjwa wa kichwa kidogo, hatahivyo chanzo chake hakitambuliki.

Post a Comment

Previous Post Next Post