Licha ya kuwa Sharon Chepchumba ni marehemu Jina lake ndilo limebeba mwito wa kampeini dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa nchini Kenya .
Wazazi wake walianza wakfu wa kuhamasisha watu kuhusu hatari za ugonjwa huo kwa jina ''Sharon live-on foundation''baada ya kumpoteza binti wao miaka kumi iliyopita .
Hii ni baada ya kuumwa na mbwa aliyekuwa na ugonjwa wa kichaa cha mbwa.
Licha ya kuwa Marehemu Sharon alipata matibabu ya dharura ilikuepuka viini vya kichaa kuenea mwilini mwake ,msichana huyo haron alikata roho wiki mbili baadaye .
Kupitia kampeini kabambe ikiwemo hatua ambazo zinachukuliwa na serikali za Manispaa au County hali ya uhamasisho kuhusu ugonjwa wa kichaa cha mbwa umeimarika maradufu nchini Kenya .
Na sio ajabu kuona matukio ya mbwa wakipashwa chanjo maeneo ya vijijini kama hali hii kaunti ya Nandi nchini kenya.
Daktari alimpatia chanjo mbwa ili kuangamiza ugonjwa wa kichaa cha mbwa
Ni eneo hili ambapo Sharon Chepchumba aliumwa na mbwa wakati wa likizo za Krisimasi mwaka wa 2003.
Kulingana na Mamake bi Agnes Korir Sharon aliumwa na mbwa sehemu ya mgongo karibu na moyo wake .
Sharon pamoja na watoto wenzake walikua juu ya mti wa mapera wakati mbwa huyo wa kike aliyeonekana kuwa na hasira alipowavamia.
Marehemu alishindwa kukimbia kuliko wenzako na akaumwa na mbwa huyo na kuambukizwa ugonjwa huo.
Baada ya kifo chake Mamake Sharon ambaye hakutaka jina la mwanawe lisahaulike alianzisha wakfu ambao unakusudia kuendeleza hamasisho kama linaloendelea Kaunti ya Nandi na kwengineko mara tu baada ya Sharon kuaga..
Nguvu zaidi zinatumiwa kuhakikisha kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa umeangamizwa kabisa
Mtaalam wa afya ya wanyama Bwana Thumi Mwangi anasema ;
''Njia ya pekee ya kuepuka ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni kupitia kuchanja mbwa wako , ama kwa njia ya haraka kujichanja baada ya kuumwa , ikiwa mbwa wako atachanjwa itakugharimu dola moja tu lakini ikiwa umeumwa na unahitaji matibabu itakugharimu dolla 100 kwa chanjo tano ambazo mtu hupashwa kipindi cha wiki mbili hivi ''
Ndio maana nguvu zaidi inatumiwa kuhakikisha kuwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa umeangamizwa kabisa sio tu eneo ambalo Sharon aliathirika bali maeneo mbali mbali kama hapa katika soko hili la mbwa magharibi mwa nchi ya kenya kwa jina Matete
Katika soko hilo wauzaji na wanunuzi wote wanahakikisha kuwa mbwa wamepata chanjo kabla ya kuondoka
Mbwa
Bwana Samuel Wambulwa-muuzaji mbwa soko la Matete anasema : Ukimnunua mbwa ni vyema apate chanjo ya kichaa cha mbwa, Nilishuhudia kifo cha Jirani wangu baada ya kuumwa na kukosa kutibiwa kwa wakati.
John Malimbe ambaye ni mteja mkubwa wa mbwa anasema: ''Ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni hatari mno na unapatikana kwa mbwa tu kwa hio tunahakikisha kuwa unapomnunua mbwa amepata chanjo kwa haraka kupitia daktari ambaye yuko maeneo haya .''
Kulingana na wataalam wa afya, watu alfu 2000 hufariki kila mwaka kutokana na kichaa cha mbwa humu nchini Kenya lakini hayo yanabadilika kutokana na kampeini kabambe ambayo imeanza kufanyika .
Kenya ina malengo ya kuhakikisha kuwa kichaa cha mbwa kinaangamizwa ifikapo mwaka wa 2030 na wakfu wa 'Sharon live-on ni mmojawapo wa harakati hizo ,ukiwa na lengo la kutimiza malengo ya shirika la Afya Duniani pamoja na mashirika mengine