BARAZA LA TIBA ASILI NA TIBA MBADALA NA MAMLAKA YA CHAKULA NA DAWA TAARIFA KWA UMMA TAREHE 16 OKTOBA, 2018 UFAFANUZI KUHUSU DAWA ZA MITISHAMBA ZIITWAZO BILLYD FOMULA POWER NA VISSION-2 ZINAZODAIWA KUTIBU MAGONJWA YA FIGO NA HOMA YA INI
1. Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ni Taasisi za Serikali zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Baraza lina wajibu wa kudhibiti usalama wa dawa asili na zinazotumika katika tiba mbadala na TFDA ina wajibu wa kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa chakula, dawa, vipodozi, vifaa tiba na vitendanishi.2. Hivi karibuni kulitolewa taarifa katika gazeti la Mtanzania, toleo Na. 9064 la tarehe 15 Oktoba, 2018 zikimnukuu Bw. Danny Njau kuwa Serikali imetoa kibali cha kusambaza na kuuza dawa zake za kutibu magonjwa ya figo na homa ya ini zijulikanazo kwa majina ya Billyd Fomula Power na Vission-2 zilizotengenezwa kwa kutumia mitishamba. Bw. Njau alinukuliwa na gazeti hilo akieleza kuwa tayari amepata vibali vyote kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Baraza, TFDA, Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
3. Taasisi za Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na Mamlaka ya Chakula na Dawa zinapenda kuutaarifu umma kuwa dawa za Billyd Fomula Power na Vission-2 zinazotengenezwa na Bw. Njau hazijathibitishwa na taasisi hizo kutibu magonjwa ya figo na homa ya ini. Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala linasajili dawa ambazo hazina madhara kwa matumizi ya binadamu lakini usajili huo haumaanishi dawa hizo zina uwezo wa kutibu ugonjwa husika.
4. Aidha, taasisi hizi hazijatoa kibali cha kutangaza dawa hizo katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kama sheria zinavyoelekeza. Matangazo ya dawa asili yanatakiwa kutolewa kwa kuzingatia Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala namba 23 ya mwaka 2002 jambo ambalo halikuzingatiwa na Bw. Njau. Page 2 of 2
5. Baraza litachukua hatua za kisheria kwa Bw. Njau kwa kutoa taarifa za kuupotosha umma kinyume na Sheria ya Tiba Asili na Tiba Mbadala, Sura Na. 244.
6. Baraza na TFDA zinatoa rai kwa watafiti, wanahabari, vyombo vya habari, watoa huduma za Tiba Asili na Tiba Mbadala na wafanyabiashara wa dawa asili nchini kuomba kibali cha Baraza kabla ya kutoa matangazo ya dawa. Endapo matangazo hayo yatatolewa bila kufuata utaratibu huo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa. Imetolewa na;
Msajili, Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,
Chuo Kikuu Dodoma,
Kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Maendeleo ya Jamii,
Jengo Na. 11, S.L.P 743 40478 Dodoma Simu: +255 26 2323267 Kaimu Mkurugenzi Mkuu,
Mamlaka ya Chakula na Dawa, Barabara ya Nelson Mandela, Mabibo, External, S.L.P 77150, Dar es Salaam.
Simu: +255 22 2452108/2450512/ 2450751/658 445222/777 700 002/ 685 701735
Hotline: 0800110084
Nukushi: +255 22 2450793
Baruapepe: info@tfda.go.tz Tovuti: www.tfda.go.tz
Tags:
ZILIZOKATAZWA