Takriban watu 140,000 hufariki duniani kutokana na ugonjwa wa surua au ukambi huku ulimwengu ukishuhudia ongezeko la maambukizi ya ugonjwa huo.
Bara la Afrika linasadikiwa kuwa na idadi kubwa zaidi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo (52,600) kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, WHO.
Surua inaweza kukingwa kupitia chanjo. Hatahivyo viwango vya maambukizi duniani vimesalia mahali pamoja kwa karibu mwongo mmoja.
Mwaka 2018, WHO lilikadiria visa milioni 2 vya ugonjwa huo huku watu karibia 52,000 wakipoteza maisha yao.
Watoto wadogo na wachanga wako katika hatari ya kupata matatizo zaidi yanayoweza kusababisha vifo.
Mwaka 2018, mashirika ya WHO na UNICEF yalikadiria kuwa asilimia 86 ya watoto duniani walipata chanjo ya kwanza kupitia mpango wa utoaji chanjo wa nchi husika, huku wengine chini ya asilimia 70 wakipata chanjo ya pili ya ugonjwa huo unaoweza kuzuiliwa.
Hata hivyo kuna haja ya idadi ya wanaopata chanjo kufika angalau asilimia 95 kwa kila nchi ili kuwa salama zaidi.
Katika kipindi cha miaka 18 iliyopita, chanjo ya ugonjwa wa surua pekee inakadiriwa kuwa kinga imara kwa zaidi ya watu milioni 23.
Barani Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Liberia, Madagascar na Somalia zimeathirika zaidi huku DRC ikiripoti visa 250,000 vya ugonjwa huo kufikia Novemba mwaka huu.
Hata ingawa mataifa maskini ndiyo yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa baadhi ya nchi zilizoendelea pia zimekuwa zikikabiliana na milipuko ya ugonjwa wa ukambi na kusababisha madhara makubwa kiafya.
Mwaka huu, Marekani imeripoti idadi kubwa ya visa vya ugonjwa wa ukambi katika kipindi cha miaka 25, huku nchi nne za Ulaya: Albania, Czechia, Ugiriki na Uingereza zikipoteza hadhi zao za kuondokana na ugonjwa huo.
Kwanini kunashuhudiwa 'janga la ghafla la surua duniani'?
Visa vya ugonjwa wa surua vilivyoripotiwa kote duniani katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka 2019 vimeongezeka mara tatu ikilinganishwa na hali ilivyokuwa wakati kama huu mwaka jana kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO).
Ni mojawapo ya virusi vinavyoambukiza pakubwa, hatahivyo hakuna kilichobadilika kuhusu ugonjwa wa surua. Sio kwamba umegeuka kuwa hatari zaidi, badala yake majibu yote yanatokana na hatua ya binaadamu.
Kuna hadithi mbili hapa - moja kuhusu umaskini na nyingine kuhusu kusambaa kwa taarifa za uongo. Katika mataifa ya kimaskini watu wachache wanapewa chanjo na sehemu kubwa ya watu wanaachwa katika hatari ya kuugua ugonjwa huo.
Hii hutoa nafasi ya kushuhudiwa mlipuko mkubwa kama ilivyoshuhudiwa katika Jamhuri ya Kidmeokrasi ya Congo, Kyrgyzstan na Madagascar.
Lakini mataifa yalio na viwango vikubwa vya utoaji chanjo yanashuhudia kuongezeka kwa ugonjwa huu. Na hii ni kutokana na kwamba baadhi ya watu wanaamua kutowapeleka watoto wapewe chanjo kutokana na kusambaa kwa taarifa za uongo katika mitandao ya kijamii dhidi ya chanjo hizo.
Ni muhimu kutambua kwamba takwimu hizi ni za awali, shirika la afya duniani linasema takwimu halisi zitakuwa juu zaidi.
Na kwamba surua au ukambi ni tishio. Husababisha vifo vya takriban watu laki moja, wengi wao watoto kila mwaka.