Matokeo ya utafiti wa damu ya mgonjwa aliyeshukiwa kuwa na virusi vya Ebola yameonyesha kwamba hana virusi vya ugonjwa huo.
Katika taarifa rasmi kwa vyombo vya habari, wizara ya afya nchini Kenya imetoa hakikisho kwamba hakuna kisa chochote cha Ebola nchini Kenya.
Waziri wa afya nchini Sicily Kariuki awali alijaribu kutuliza wasiwasi uliopo kwa kueleza kwamba dalili za mgonjwa aliyeshukiwa kuwa na Ebola 'haziambatani na ugonjwa huo'.
Mwanamke aliyeshukiwa kuwa na Ebola alitengwa katika Hospitali ya Kericho, eneo la Bonde la Ufa kusini-magharibi mwa Kenya.
Bi Kariuki ameeleza kwamba ukaguzi unaofanywa ni hatua ya tahadhari.
"Dalili za mgonjwa haziambatani na ugonjwa wa Ebola ," amewaambia wandishi habari katika uwanja mkuu wa ndege Nairobi alikofanya ukaguzi wa vituo vya udhibiti wa Ebola.
Sampuli za damu za mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 36zimeonyesha kamba hana virusi vya Ebola.
Mumewe na watu wengine wawili walio karibu naye pia walitengwa.
Maafisa wa afya katika Kaunti ya Kericho wamesema kuwa mwanamke huyo anayekaguliwa alisafiri kutoka Malaba eneo la mpaka kati ya Kenya na Uganda.
Hakuna ripoti yeyote iliyotolewa ya kuwepo kwa ugonjwa wa Ebola karibu na mpaka wa Malaba:Isipokuwa eneo la Magaharibi mwa Uganda.
Mgonjwa huyo alikwenda hospitali binafsi siku ya Jumapili alikua na homa, maumivu ya kichwa,maumivu ya viungo,maumivu ya koo na alikua akitapika.
Alitibiwa malaria kwenye hospitali ndogo lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya .
Alifanyiwa tena kipimo cha malaria na majibu yalionyesha hana malaria.Kutokana na hali hiyo wahudumu wa afya walimpa rufaa kwenda hospitali ya Kaunti ya Kericho ambayo ina uwezo wa kuweka karantini.
Baadae akaanza kuharisha ambapo sasa taarifa zinasema anaendelea vyema.
Matokeo ya awali ya vipimo yanatarajiwa kuwa tayari katika kipindi cha saa 12 mpaka 24.
Idara ya huduma za afya ya kaunti ya Kericho imesema inafuatilia kwa karibu suala hili na inafanya kazi pamoja na serikali kuu kuhakikisha kuwa hatua madhubuti zinafuatwa kuhakikisha usalama wa kiafya kwa wengine.
Serikali ya Kaunti imeuhakikishia Umma kuwa hospitali ya kaunti ina uwezo na ina vifaa kuhakikisha mgonjwa anatengwa na kuwalinda watumiaji wengine wa hospitali na imetoa wito kwa watu kuwa watulivu na wenye subira.
Ebola Uganda
Juma lililopita Mtoto wa miaka mitano nchini Uganda alipatikana kuwa na Ebola, shirika la afya duniani (WHO) lilithibitisha.
Uthibitisho kwamba ni ugonjwa wa Ebola ulitolewa na taasisi ya kupambana na virusi nchini Uganda Virus Institute (UVRI) Jumanne juma lililopita baada ya kutangazwa rasmi na maafisa.
Wizara ya afya nchini Uganda na WHO walituma kikosi maalum kutambua wengine walio katika hatari, taarifa ya pamoja ilieleza.
Waziri wa afya Uganda Jane Ruth Aceng aliwaambia waandishi wa habari kwamba familia ya mtoto huyo inaangaliwa, wakiwemo wawili walioonyesha kuwa na dalili za kama za ugonjwa wa Ebola.
Baada ya hapo alituma ujumbe kwenye Twitter akieleza kwamba nchi hiyo imeingia katika 'hali ya muitikio'kufuatia kisa hicho.
Taarifa za baadae zilisema kuwa mtoto huyo alipoteza maisha
Tayari wahudumu 4, 700 nchini Uganda wamepewa chanjo dhidi ya ugonjwa huo, taarifa hiyo ya pamoja ya Shirika la afya duniani na wizara ya afya nchini Uganda ilithibitisha.
Tahadhari Tanzania
Watanzania wametakiwa "wasiwe na hofu" kuhusu kusambaa kwa Ebola. Waziri wa afya Ummy Mwalimu alisema baada ya taarifa za Ebola kuingia Uganda kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mpaka wa Tanzania unashikana na wa Congo, ambako virusi vya ugonjwa huo vimesababisha vifo vya takriban watu 1, 400.
Kauli hii ilitolewa wakati Uganda ikithibitisha kwamba kuna visa saba vya watu wanaoshukiwa kuugua ugonjwa huo nchini Uganda
Katika ujumbe kwenye mtandao wa Twitter, Bi Mwalimu amesema Tanzania "imekuwa ikichukua hatua za utayari wa kukabiliana na ugonjwa huu".
Zaidi ya watu 2,000 waugua Ebola nchini DRC
Zaidi ya watu 2,000 wameripotiwa kuugua ugonjwa wa Ebola nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika kipindi cha miezi 10, maafisa wameeleza.
Theluthi mbili walikua kwenye hali mbaya zaidi, wizara ya afya ilieleza.
Mlipuko wa ebola ni wa pili kwa ukubwa nchini DRC, kukiwa na ripoti ya kutokea maambukizi mapya wiki za hivi karibuni.
Lakini wafanyakazi wa afya waliripoti kupata vikwazo vya kutoaminika na machafuko nchini humo.
Watu wengine hawawaamini watoa huduma za afya, hivyo hufanya watu wenye dalili za ugonjwa huo kukwepa matibabu, hali hii inawia vigumu kuzuia kuenea kwa virusi vya ebola.
Ingawa zaidi ya watu 1,300 wamepoteza maisha tangu mwezi Agosti, Shirika la misaada la Oxfam linasema linakutana na watu kila siku ambao hawaamini kama kuna virusi vya ebola.Mhariri wa BBC Africa Will Ross anaripoti.
Ebola ni nini?
Ni ugonjwa unaosambaa haraka na kusababisha vifo vya asilimia 50 ya waathirika
Dalili za awali ni homa ya ghafla, uchovu kupita kiasi, maumivu ya mishipa na koo.
Dalili za hatari ni kutapika, kuharisha, na kwa kesi zingine ni kutoka damu ndani na nje ya mwili.
Ebola huwapata binadamu wanapo gusana na wanyama walio athirika wakiwemo sokwe mtu, popo na paa.
Watu wanaambukiza endapo damu zao na maye vimebeba vijidudu, na hii inaweza fika mpaka wiki saba tangu mtu alipopona.