Watafiti wameonya kuhusu athari za kiafya zinazoweza kupatikana kutokana na matumizi ya simu na fedha chafu.
Fedha, haswa ya sarafu, wanasayansi wanasema kwamba vimelea vya magonjwa kama ya kuhara na magonjwa mengine mengi ambayo yanaweza kupatikana katika katika chakula ni rahisi mtu kupata.
Utafiti huo ambao ulifanywa kwa wauza chakula wapatao 395 katika maeneo tofauti tofauti ya jiji la Nairobi, nchini Kenya na wataalamu kutoka chuo cha Kilimo na teknolojia, Taasisi ya utafiti wa dawa na watafiti kutoka Marekani, umeonyesha kuwa vimelea vinavyopatikana katika simu pamoja na fedha hutengeneza sumu katika chakula.
Walifanya uchunguzi wa sarafu ambazo zinazunguka sana ndani ya Nairobi na ripoti ilibaini kuwa shilingi 5, 10 na 20 ndio zilikuwa chafu zaidi ikifuatiwa na shilingi 50, 100 na 200.
Pesa nyingi ambazo zinazunguka sana na simu zilikutwa na vimelea vidogo vinavyoambukiza magonjwa.
Jambo baya zaidi katika migahawa au maeneo yanayouza chakula, haswa wahudumu na wapishi kutokuzingatia usafi baada ya kutumia simu zao.
Wakati wa utafiti, washiriki 34 walikutwa wagonjwa huku wengine wakiwa wanasumbuliwa na kikohozi, magonjwa ya tumbo na homa.
Magonjwa haya yalikuwa hayawasumbui wagonjwa peke yake, lakini pia yalikuwa yanasambaa katika chakula ambacho mhudumu wa chakula au mpishi alikuwa anakiandaa.
Hata hivyo, zaidi ya asilimia 60 walikuwa hawajaosha mikono yao baada ya kushika pesa au kutumia simu.
Kwa kawaida, inatakiwa mpokeaji chakula asiwe yule anayehudumia chakula ila imezoeleka kwa wengi, mpishi au mhudumu wa chakula kuwa ndio mtu anayepokea pesa.
"Wauzaji chakula na umma kwa ujumla wanapaswa kuzingatia hatari ambazo zinaweza kujitokeza wakati wanapata chakula mara baada ya kushika pesa au simu zao za mkononi," utafiti umeonya.
Mwaka 2009, utafiti wa namna hiyo ulifanyika jijini Nairobi na kubaini kuwa pesa huwa zinasambaza vimelea vingi vya magonjwa.
Sarafu zilizokuwa na kiwango kikubwa cha vimelea zilikuwa zimetoka katika bucha, wauza chakula pembezoni mwa barabara kama wachoma mahindi na katika migahawa midogo.
Kwa mujibu wa mtafiti Dkt.Richard Korir kutoka kituo cha utafiti cha Kemri, amesema kuwa vimelea hivyo vya magonjwa vinaenea kwa haraka kwa sababu watu hawasafishi mikono yao na kutozingatia usafi wa mazingira yanayowazunguka na hivyo kusababisha bakteria kuenea katika chakula.
Utafiti mwingine uliangalia bakteria aina tofauti tofauti ambao wanapatikana katika mazingira , chakula vyombo na ngozi za watu pamoja na wanyama.
Licha ya kwamba bakteria hao huwa hawana madhara makubwa lakini wengine husababisha magonjwa ya tumo, chakula kuwa na sumu na kusababisha magonjwa ya ngozi.
Kama ukilinganisha pesa na simu, pesa ndio hatari zaidi.
"Watu wengi hawaoni kwamba kushika simu ni sawa na kushika uchafu hivyo inawapelekea kupata maambukizi , kwa kushindwa kuosha mikono yao baada ya kutumia simu" alisema Dkt.Korir.