gharama za kupima dengue zapungua:Serikali ya TANZANIA.

Serikali imeleta vitendanishi vya maabara kwa ajili ya ugonjwa wa homa ya dengue na kupunguza gharama za vipimo vya maradhi hayo mpaka kufikia Sh15,000.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema jana kuwa vipimo hivyo vimeshawasili na kusambazwa katika vituo vilivyotengwa kufuatilia ugonjwa huo.

“Tumeleta vipimo vya maabara vya kutosha na vingine vipo njiani na sasa bei imeshuka itakuwa kati ya Sh15,000 mpaka Sh20,000,” alisema Dk Ndugulile.

Vituo ambavyo vipimo hivyo vitapatikana ni hospitali za Mwananyamala, Ilala, Temeke na vijibweni kwa Dar es Salaam na Hospitali ya Bombo, Tanga.

Tangu Januari hadi sasa, wananchi wamekuwa wakitumia kati ya Sh40,000 hadi Sh65,000 katika hospitali binafsi kupima virusi vya homa hiyo ambayo hadi sasa waliothibitika kuugua wamefikia 1,237.

Neema Mushi ambaye ameugua homa hiyo alisema jana kuwa gharama za vipimo hivyo ni kubwa na hata mifuko ya bima za afya haisaidii, “nina bima mbili, lakini zote niliambiwa haziwezi kutumika nilitoa fedha mfukoni. Wapo walioshindwa kupima kutokana na kukosa fedha.”

Akizungumzia gharama, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi alisema wizara inatambua kuwa upimaji wa ugonjwa huo kwa sasa ni ghali hasa katika vituo binafsi vya kutolea huduma.

Alisema wizara inawasiliana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili kuona namna ya kuuingiza ugonjwa huo katika bima.

“Tunalishughulikia suala hilo kwa kuhakikisha tunaimarisha upatikanaji wa huduma za upimaji kwa gharama nafuu kwenye vituo vyetu vya umma na tumeshandaa mwongozo wa matibabu kwa ajili ya watoa huduma katika vituo vyetu,” alisema.

Alisema Serikali imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kuendelea kuangamiza mazalia ya mbu katika jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine.

Alisema tayari wameandaa mpango wa dharura wa miezi sita kutoka Mei hadi Oktoba mwaka huu kukabiliana na ugonjwa huo.

“Tumenunua vitendanishi vyenye uwezo wa kupima wagonjwa 1,870 na vimeshasambazwa kwenye vituo maalumu vya ufuatiliaji... ununuzi zaidi wa vitendanishi unaendelea kadri ya uhitaji kwenye vituo vya kutolea huduma,” alisema.

Kikosi kazi kudhibiti mbu

Mganga mkuu huyo wa Serikali alisema wizara imeanzisha kikosi kazi cha wataalamu kwa ajili ya kushughulikia udhibiti wa mbu wanaoeneza ugonjwa wa dengue na malaria nchini na kinaendelea na kazi ya kuhamasisha jamii.

“Tunaendelea kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa ugonjwa wa dengue uliopo kwenye vituo maalumu.”

Mkurugenzi wa huduma za Kinga Wizara ya Afya, Dk Leonard Subi alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha bei ya vipimo vya homa ya dengue inapungua na wananchi wote wanaohisiwa wanamudu kupima.

“Lengo letu ni kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa. Tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo wa ugonjwa huu.”

Post a Comment

Previous Post Next Post