Serikali ya Tanzania imetoa msaada wa dawa, chakula na vifaa vya kujihifadhi kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa kimbunga cha Idai kilichosababisha mafuriko yaliyozikumba nchi hizo tangu wiki iliyopita.
Msaada huo umekabidhiwa kwa Mabalozi wa nchi hizo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya msaada huo utapelekwa nchi za Zimbabwe na Msumbiji unatarajiwa kusafirishwa kwa kutumia ndege za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Akizungumza wakati zoezi la kupakia msaada huo katika ndege ya Jeshi likiendelea Mhe. Prof. Kabudi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameagiza kutolewa kwa msaada huo sambamba na salamu za pole kwa Marais wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe pamoja na wananchi wa nchi hizo kwa madhara makubwa waliyoyapata kutokana na mafuriko hayo.
"Rais Magufuli baada ya kupata taarifa hizi na kuzungumza na Marais wenzake wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, Tanzania imeona ni vyema kutokana na undugu wetu, umoja wetu na ujirani wetu tuweze kuwapelekea msaada angalau kidogo wa dawa na chakula na pia kuwapa pole kwa maafa haya makubwa yaliyowapata" amesema Prof. Kabudi.
Idadi ya watu waliofariki kutokana na kimbunga Idai nchini Msumbiji sasa huenda ikawa ya juu na kufikia watu 1000 rais Filipe Nyusi amesema.
Bwana Nyusi alisafiri kwa ndege katika maeneo yalioathirika zaidi siku ya Jumatatu. Alielezea kuona miili ikielea juu ya mito.
Tayari kuna hatari ya maisha ya zaidi ya watoto 100,000 na watu wazima kufuatia kikmbunga hicho huku mito katika maeneo yaliothirika zaidi ikivunja kingo zake , kulingana na shirika la Save the Children.
Mafuriko yaliofanyika mapema mwezi huu yamezidishwa na kimbunga Idai ambacho kilikumba eneo la kaskazini mwa Msumbiji mnamo tarehe 15 mwezi Machi 2019 na kusababisha unahiribifu mkubwa wa nyumba , shule, hospitali na miundo mbinu.
Kulingana na serikali ya Msumbiji takriban watu 600,000 wameathiriwa , huku maisha ya zaidi ya watu 1000 yakidaiwa kupotea huku yale ya watu 100,000 yakihitaji msaada wa dharura mjini Beira.
Kiwango cha janga hilo kinazidi kuongezeka kila dakika na shirika la Save the Children lina wasiwasi mkubwa kuhusu watoto na familia walio katika hatari huku viwango vya mafuriko vikizidi kuongezeka anasema Machel Pouw mkuu wa operesheni ya shirika hilo nchini Msumbiji.
Kimbunga hicho kilishuka katika mji wa bandari wa Beira siku ya Alhamisi kikiwa na upepo wenye kasi ya hadi kilomita 177 kwa saa , lakini mashirika ya misaada yalifika katika eneo hilo siku ya Jumapili.
Mfanyikazi mmoja wa Umoja wa mataifa aliambia BBC kwamba kila nyumba mjini Beira- ambapo ni mji wenye makaazi ya watu nusu milioni iliharibiwa.
Gerald Bourke, kutoka kwa shirika la chakula duniani , alisema: Hakuna nyumba ambayo haikuathiriwa . hakuna Umeme, hakuna mawasiliano.
Barabara zimejaa magogo ya nyaya za umeme. Paa za nyumba zimeanguka pamoja na nyuta zake. raia wengi wa mji huo wamepoteza makaazi yao.
Idadi rasmi ya watu waliofariki nchini Msumbiji inadaiwa kuwa watu 84 kufuatia mafuriko na upepo mkali.
Kimbunga hicho kimewaua takriban watu 180 katika eneo lote la Afrika Kusini.
Shirika la msalaba mwekundu limeelezea uharibifu huo kuwa mbaya zaidi na wa kutisha. Watu wamelazimika kuokolewa wakiwa juu ya miti , Jamie LeSeur mkuu wa IFRC aliambia BBC.
Nchini Zimbabwe takriban watu 98 wamefariki huku 217 wakiwa hawajulikani waliko mashariki na kusini serikali imesema.
Idadi ya watu waliofariki inashirikisha wanafunzi wawili wa shule ya St Charles Lwanga katika wilaya ya Chimanimani, ambao walifariki baaada ya bweni lao kuathiriwa kutokana na mawe yaliosombwa na maji hayo katika mlima.
Malawi pia nayo iliathiriwa vibaya . Mafuriko nchini humo yaliosababishwa na mvua kabla ya kimbunga hicho kuwasili yalisababisha mauaji ya vifo 122 kulingana na mitandao ya mashirika ya misaada.
Serikali ya Uingereza inasema kuwa itatoa msaada wa kibinaadamu wenye thamani ya £6m kwa Msumbiji na Malawi.
Pia imesema kuwa itatuma mahema pamoja na maelefu ya mahema nchini Msumbiji.
Uharibifu wa Beira ni mkubwa kiasi gani?
Wengi wa wale wanaojulikana kufariki waliuawa karibu na mji wa Beira , ambao ndio mji mku wa nne kwa ukubwa ukiwa na idadi ya watu isiopungua nusu milioni kulingana na mamlaka.
Zaidi ya watu 1500 walijeruhiwa na miti pamoja na vifusi vilivyoanguka ikiwemo paa , kulingana na maafisa katika mji mkuu wa Maputo waliozunguzma na BBC.
''Karibu kila kitu kimeathiriwa na janga hili'' , Alberto Mondlane , gavana wa mkoa wa Sofala unaoshirikisha Beira alisema siku ya Jumapili. Tuna watu wanaotaabika kwa sasa , wengine juu ya miti na wanahitaji sana msaada.
''Wakaazi wa Beira wamefanya juhudi za kujaribu kufungua barabara za mji huo'', bwana LeSeur aliambia BBC.
Barabara inayounganisha Beira na maeneo mengine ya taifa hilo iliharibiwa vibaya, lakini usafiri wa ndege hadi maeneo yalioathirika pakubwa umeanzishwa.
Rais Filipe Nyusi alikata ziara yake ya Swaziland ili kutembelea maeneo yalioathirika.
Je hali ikoje nchini Zimbabwe?
Hali ya janga imetangazwa nchini Zimbabwe . Rais Emmerson Mnangagwa amerudi nyumbani mapema kutoka kwa ziara ya kuelekea UAE ili kuhakikisha kuwa anashiriki moja kwa moja katika janga hilo la kitaifa , mamlaka imesema.
Wizara ya habari imesambaza picha za wanafunzi kutoka shule ya St Charles Lwanga , ambao kwa sasa wameokolewa.
Manusura katika hospitali moja katika wilaya ya Chimanimani walizungumza kuhusu vile mafuriko hayo yalivyoharibu nyumba zao na kuwasomba wapendwa wao.
''Hadi sasa sijui ni wapi mwangu yupo'' , Jane Chitsuro aliambia shirika la habari la AFP . ''hakuna samani , hakuna nguo ni vifusi na mawe pekee'.
Nyumba ya Praise Chipore pia nayo iliharibiwa .
''Mwanangu alikuwa nami kitandani akasombwa na mafuriko huku mafuriko makubwa yakinisomba mie pia'', alisema.
Je umewahi kuona tukio kama hili hapo awali
Mwandishi wa BBC Shingai Nyoka, nchini Zimbabwe anaripoti.
Safari yangu kuelekea Chimanimani iliisha ghafla wakati tulipofika katika eneo hili .
Maji ya mto yalikuwa yakipita kwa nguvu huku watu kadhaa wakiwa wamesimama katika pande mbili za daraja hili.
Hii ndio iliokuwa barabara kuu iliokuwa ikiunganisha mji wa Mutare kuelekea kijiji cha Chimanimani ambayo imekatwa .
Mashirika ya misaada yameshindwa kufika katika eneo hilo. Wakaazi wanaoishi katika eneo hilo wanasema kuwa hawajashuhudia tukio kama hilo.
Wanandoa wawili walio na umri mkubwa , Edson na Miriam Sunguro waliniambia kwamba wamejaribu kuwasiliana na wapendwa wao katika eneo la Chimanimani bila mafanikio.
Je hali ya hewa itabadilika?
"Kuna hatari ya mvua kubwa zaidi kunyesha katikja kipindi cha siku chache zijazo katika eneo la kaskazini mwa Msumbiji pamoja na kusini mwa Malawi , kulingana na mwandishi wa hali ya hewa wa BBC Chris Fawkes says.
Huenda kukawa na ngurumo za radi , aliongezea, lakini kuna picha za mawingu yaliowachwa na Kimbunga idai ambayo huenda yakazuia ngurumo za radi kuanza.