Wanawake wengi miaka ya karibuni wanakabiliwa na tatizo linalofanana na kitambi kwa upande wa wanaume. Hivyo ingekuwa ni wanaume tungesema ni kitambi ambalo nalo ni tatizo kubwa miongoni mwa wanaume wengi nyakati za sasa.
Kinachowasumbuwa wanawake siyo kitambi tunasema ni mlundikano wa mafuta sehemu ya chini ya tumbo na tumbo kwa ujumla kufikia hali kuonekana kama ana tumbo kubwa au kuhisi labda ni ujauzito kumbe ni mafuta tu mengi.
Kwa ujumla ni vigumu sana kupunguza tumbo la namna hii, hivyo kwenye post hii pamoja na mengine tutaona pia visababishi vya tatizo lenyewe, dawa za asili zinazoweza kuondoa tatizo hilo na aina ya maisha unayotakiwa kuishi ili ufanikiwe kirahisi zaidi bila kukuachia madhara mengine yoyote.
Nini kinasababisha tumbo kwa kina mama:
Vyakula feki (Junk food)
Kutumia vyakula vya wanga kupita kiasi
Kutokunywa maji ya kutosha kila siku
Kula chakula kizito muda mchache kabla ya kwenda kulala
Kukaa masaa mengi kwenye kiti
Kutokujishughulisha na mazoezi
Mfadhaiko (stress)
Kula wali kila siku
Ugali wa sembe
Kula vyakula vinavyopikwa katikati ya mafuta mengi (chipsi, maandazi, nk)
Vyakula vinavyoondoa mafuta kwenye tumbo kwa wanawake
mbegu-za-maboga
1. ASALI NA LIMAU
Chukua asali kijiko kikubwa kimoja cha chakula na majimaji ya limau vijiko vikubwa viwili, changanya hivi viwili ndani ya glasi moja (robo lita) ya maji ya uvuguvugu na unywe yote mara tu ukiamka asubuhi.
Tumia kwa wiki 3 hivi mpaka mwezi mmoja na hutachelewa kuona tofauti.
2. MAJI YA UVUGUVUGU
Kunywa maji ya uvuguvugu kama lita 1 hivi wakati tumbo likiwa tupu hasa asubuhi ukiamka tu. Hii inasaidia kusafisha mwili na kuondoa mafuta yasiyohitajika.
3. NYANYA
Kula nyanya ambazo hazijapikwa pia inasaidia kupunguza tumbo kwa kina mama, hivyo kula kachumbali ya kutosha kila siku ya nyanya peke yake na utaona mabadiliko.
4. TANGAWIZI
Chemsha chai ya tangawizi, ipua na usubiri ipowe kidogo, ongeza asali mbichi kidogo na pilipili manga kidogo ya unga. Pata kikombe kimoja cha chai hii kila siku asubuhi mapema ukiamka tu. Asali inasaidia kuyeyusha mafuta wakati pilipili itauongezea nguvu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
5. SIKI YA TUFAA
Siki ya tufaa (apple cider vinegar) inasaidia kupunguza njaa na kukufanya ujisikie umeshiba kwa kipindi kirefu. Kunywa kijiko kikubwa kimoja cha siki ya tufaa mara 1 kwa siku kila siku wakati unakula chakula cha usiku. Kazi nyingine ya hii siki ni kuweka sawa damu sukari mwilini hivyo ni nzuri pia kwa wenye kisukari.
6. MAJANI YA BIZARI
Majani ya bizari husaidia kuondoa sumu na takataka nyingine mwilini kitu ambacho moja kwa moja hupelekea mlundikano mdogo wa mafuta katika tumbo. Kunywa chai ya majani ya bizari kila siku asubuhi, ukikosa majani unaweza kutumia hata unga wake.
8. ILIKI
Iliki hufanya kazi ya kuongeza nguvu katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na ni dawa nzuri sana ya kuondoa sumu na takataka nyingine mwilini. Iliki pia hutumika katika kupunguza uzito. Tengeneza chai yenye iliki kila siku ndani yake, pia ni kiungo karibu kwa vyakula vingi hivyo hakikisha unaiweka katika kila chakula unachopika kwa matokeo mazuri zaidi.
9. MDALASINI
Mdalasini hufanya kazi ya kuchoma mafuta mwilini. Chukua kijiko kidogo kimoja cha mdalasini ya unga na uweke ndani ya glasi 1 ya maji ya moto na uache kwa dakika 5 hivi. Ongeza kijiko kidogo kimoja cha asali mbichi ndani yake na ukoroge vizuri, kisha unywe huo mchanganyiko wote asubuhi ukiamka tu.
10. JUISI YA LIMAU
Kunywa maji ya limau au juisi ya limau kila mara kutakusaidia kuondoa mafuta tumboni kwa haraka sana. Ongeza majimaji ya limau vijiko vikubwa viwili ndani ya glasi 1 ya maji na uongeze punje 1 ya chumvi ya mawe, koroga vizuri na unywe asubuhi ukiamka tu kila siku.
11. KITUNGUU SWAUMU
Ili kupunguza mafuta tumboni katakata vipande vidogo vidogo (chop) punje 3 mpaka 4 za kitunguu swaumu na unywe na maji vikombe viwili asubuhi tu na kisha shushia na glasi moja ya maji yenye limau kidogo kwa mbali. Hii ndiyo njia nzuri kabisa ya asili ya kuondoa mafuta tumboni kwa haraka zaidi.
12. TIKITI MAJI
Tikiti maji lina asilimia 82 za maji kitu kinachofanya tumbo lako kutokuwa na njaa ya kuhitaji chakula. Tikiti maji lina vitamini C ambayo ni mhimu kwa afya bora. Kula tikiti kila siku.
13. MAHARAGE
Kula maharage kila mara kunasaidia kupunguza mafuta katika tumbo. Maharage yana kiasi kingi cha nyuzinyuzi (faiba) kitu kinachosaidia tumbo lako kutojisikia njaa na hivyo itakuwezesha kula chakula kiasi kidogo. Kadri unavyokula chakula kichache ndivyo unavyokuwa mbali na uwezekano wa kuzalisha mafuta mengi tumboni.
Basi kula maharage kila siku.
14. TANGO
Tango lina asilimia 96 za maji na asilimia zinazobaki ni nishati. Tumia kachumbali yenye tango ndani yake kila siku au kula tu tango moja kila siku ili kupunguza mafuta tumboni kwa haraka.
15. PARACHICHI
Parachichi ni tunda lingine zuri sana kwa ajili ya kuchoma mafuta yaliyozidi mwilini. Parachichi ni chanzo kizuri cha nyuzinyuzi (faiba). Parachichi huikimbiza mbali njaa na wewe. Parachichi lina mafuta lakini ni mafuta mazuri (monounsaturated fatty acids) ambayo yenyewe husaidia kuchoma mafuta na hivyo kuondoa mafuta mabaya tumboni kirahisi zaidi.
Kula parachichi 1 kila siku.
16. TUFAA
Kula tufaa maarufu sana kama ‘apple’ (epo) kunaweza kusaidia kupigana na magonjwa mengi sana mwilini na inaweza pia kusaidia kuondoa mafuta kwenye tumbo lako. Tufaa hukufanya ujisikie umeshiba sana kwa masaa mengi sababu lina potasiamu na vitamini nyingi sana ndani yake.
Hivyo kula tunda hili 1 kila siku asubuhi kupunguza shauku yako ya kutaka kula zaidi ndani ya hiyo siku nzima.
17. MAFUTA YA SAMAKI
Mafuta ya samaki ni mbadala mzuri kabisa katika kuchoma mafuta ya tumboni. Mafuta ya samaki yenyewe hulenga kuyachoma moja kwa moja mafuta yanayozidi tumboni. Ukiweza unaweza kuamua yawe ndiyo mafuta yako ya kupikia, pia unaweza kunywa mafuta haya kijiko kikubwa kimoja kila siku unapoenda kulala.
18. SIAGI YA KARANGA
Siagi ya karanga hupunguza njaa na kuongeza nguvu katika mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Siagi ya karanga ina kiinilishe kijulikanacho kama ‘niacin’ ambacho chenyewe huzuia mafuta kujilundika tumboni. Hivyo kwenye mkate wako asubuhi ningekushauri utumie hii siagi ya karanga badala ya mafuta mengine ambayo si salama, pia unaweza kutumia hii siagi ya karanga kama mafuta yako ya kuunga katika mboga nyingi unazopika hata katika wali unaweza kutumia kama mafuta yako mbadala.
19. MAYAI
Mayai yana vitamini nyingi sana ndani yake (mayai ya kienyeji lakini) na yana madini pia kama kalsiamu, zinki, chuma, omega -3 nk. Viinilishe vyote hivyo katika mayai husaidia kuchoma mafuta yanayozidi tumboni. Hivyo kula mayai asubuhi kila siku ili kuondoa na kupunguza mafuta mwilini. Mayai pia ni moja ya vyakula vinavyomfanya mtu ajisikie kushiba kwa muda mrefu bila kuhitaji kula kula tena.
20. CHAI YA KIJANI
Chai ya kijani maarufu kama ‘Green tea’ hufanya kazi ya kuondoa sumu mwilini jambo linalosaidia pia kuchoma mafuta yaliyozidi mwilini. Kunywa chai hii ya kijani kila siku kutafanya ngozi yako kukua vivyo hivyo kufanya tumbo lako kukaa sawa bila kuwa na mafuta mengi.
21. MTINDI
Ingawa mtindi unaweza kupelekea kuongeza uzito zaidi, hata hivyo mtindi mtupu kabisa ule ambao haujaongezwa kingine chochote ndani yake unaweza kukusaidia kupunguza mafuta tumboni. Matumizi yake kwa siku yasizidi kikombe kimoja (robo lita). Pia mtindi ni moja ya vyakula vinavyoweza kukufanya ujisikie umeshiba na hivyo kukuondolea njaa ya kutaka kula.
22. JUISI YA KOTIMIRI
Juisi ya kotimiri (Parsley juice) huondoa sumu na takataka nyingine zozote mwilini, pia huchoma mafuta na nishati. Kotimiri ni dawa nzuri kwa matatizo mbalimbali ya figo pia kwa kuchoma mafuta mwilini.
Pata kikombe kimoja cha juisi hii kila siku unapoenda kulala.
23. NDIZI
Kama lilivyo tufaa, ndizi pia zina kiasi kingi cha potasiamu na vitamini za aina mbalimbali ndani yake. Ukipenda kula ndizi kila mara zinachofanya mwilini mwako ni kuondoa ile hamu ya kutaka kula vyakula feki (fast food). Zaidi sana ndizi huuongezea nguvu mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na hivyo kupelekea mafuta ya tumboni kuyeyuka kirahisi zaidi. Kula ndizi kila siku ukiweza ukiamka tu kula ndizi zilizoiva 3 mpaka 5 kila siku.
mbegu-za-maboga
24. MAJI YA KUNYWA
Kunywa maji ya kutosha kila siku kunasaidia pia kupunguza uzito. Kunywa maji lita 2 mpaka 3 kila siku iendayo kwa Mungu. Kunywa maji kidogo kidogo kutwa nzima. Hili halitafanya kazi ya kusafisha mwili tu bali pia litafanya ngozi yako kung’aa na kukuwa. Nywele zako pia zitaonekana ni zenye afya na mwili mzima utakuwa ni wenye kuvutia.
Kitu cha kwanza ukiamka tu ni kunywa maji glasi 2 na uendelee hivyo hivyo glasi moja moja kila baada ya lisaa limoja au mawili kutwa nzima. Maji ni uhai, bila kunywa maji kila siku ni sawa na kwenda dukani bila hela mfukoni.
Asilimia 94 ya damu yako ni maji, asilimia 85 ya ubongo wako ni maji, asilimia 27 ya mifupa yako ni maji, asilimia 75 ya mwili wako ni maji. Sehemu kubwa ya dunia hii imefunikwa na maji na sehemu yenye ardhi ni kipande kidogo sana. Haijalishi unaishi kwenye baridi au kwenye joto hakikisha unakunywa maji ya kutosha kila siku, huhitaji kusikia kiu au hamu ndipo unywe maji, hapana maji ni lazima uyanywe tu hata iweje.
25. MAZOEZI YA KUTEMBEA
Shida kubwa kwa kina mama wengi wa kiTanzania ni kuwa hawajishughulishi na mazoezi. Hapa Tanzania mazoezi inaonekana ni jambo la wanaume tu. Mazoezi ni jambo la lazima kwa mtu yeyote iwe unaumwa au huumwi.
Ili kuchoma mafuta mwilini kwa haraka zaidi tembea kwa miguu mwendo kasi kidogo lisaa limoja kila siku. Kumbuka nimesema lisaa limoja yaani dakika 60 bila kupumzika (none stop) kila siku. Kutembea kwa miguu lisaa limoja huamsha mwilini kimeng’enya kijulikanacho kama ‘lipase’ ambacho chenyewe huamka tu ikiwa utatembea bila kusimama kwa dakika 60 na kikishaamshwa (when it is activated) huendelea kuchoma mafuta mwilini kwa masaa 12 mfulululizo.
Usiseme nikitoka sehemu fulani kwenda sehemu fulani nitakuwa nimetembea vya kutosha, hapana, unahitaji uwe na saa mkononi kuhakikisha kweli dakika 60 zimeisha ukiendelea kutembea bila kusimama. Kama utaweza kukimbia kidogo kidogo (jogging) basi utachoma mafuta ya tumbo kwa haraka zaidi.
Ufanye zoezi hili kila siku kwa mwezi mmoja mpaka miwili mfululizo na mafuta kwenye tumbo lako yatapotea yenyewe bila kupenda.