Maafisa wa afya katika jimbo la Kerala, kusini mwa India wamethibitisha kwamba watu tisa wamefariki kutokana na kinachodhaniwa kuwa virusi hatari vya Nipah.
Watatu walikuwa wamepatikana na virusi hivyo katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.
Matokeo ya wengine sita yatatolewa baadaye Jumatatu.
Watu wengine 25 wamelazwa hospitalini wakiwa na dalili za ugonjwa huo eneo la Kozhikode, maafisa wanasema.
Nipah ni ugonjwa ambao unaweza kuambukiwa binadamu kutoka kwa wanyama.
Hakuna chanjo yoyote ya ugonjwa huo kwa sasa.
Asilimia 70 ya wanaoambukizwa virusi hivyo hufariki dunia.
Virusi vya Nipah vimo miongoni mwa orodha 10 ya magonjwa ambayo yanaangaziwa zaidi na Shirika la Afya Dunia (WHO). Magonjwa hayo yametambuliwa kuwa miongoni mwa magonjwa yenye uwezo wa kusababisha mlipuko mbaya sana wa ugonjwa karibuni.
Waziri wa afya wa Kerala Rajeev Sadanandan ameambia BBC kwamba mwuguzi aliyewatibu wagonjwa hao pia amefariki.
"Tumepeleka damu na majimaji ya mwili kutoka kwa wanaoshukiwa kuambukiwa kwa Taasisi ya Taifa ya Virusi mjini Pune zikapimwe. Kufikia sasa, tumethibitishiwa kwamba watatu walifariki kutokana na virusi hivyo vya Nipah," amesema.
"Sasa tunaangazia kuchukua tahadhari kuzuia kuenea kwa ugonjwa huu kwa sababu hatua zozote ambazo zinaweza kuchukuliwa ni kuwatunza wanaougua."
Popo wa matunda, ambao hula matunda, wanaaminika kuwa vimelea (wanyama wanaobeba virusi hivyo bila kudhuriwa navyo).
Maafisa wa afya wanasema walipata maembe ambayo yameumwa na popo hao nyumbani kwa watu watatu waliofariki baada ya kuambukizwa.
Virusi vya Nipah virus?
- Virusi vya Nipah ni ugonjwa mpya ambao unaanza kuenea karibuni ambao unaweza kuenezwa kutoka kwa wanyama hadi kwa binadamu. Kimelea chake ni popo wa matunda.
- Maambukizi ya kwanza ya ugonjwa huo yalitambuliwa 1999 wakati wa mlipuko wa ugonjwa mwingine ulioathiri wafugaji wa nguruwe Malaysia na Singapore.
- Karibu visa 300 vya binadamu kuambukizwa, na watu zaidi ya 100 kufariki viliripotiwa baada ya mlipuko huo. Nguruwe zaidi ya milioni moja waliuawa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo.
- Maambukizi ya virusi vya Nipah yanawezakuzuiwa kwa kupunguza kukutana na nguruwe wanaougua au popo
- Dalili zake ni pamoja na homa kali, kuumwa na kichwa, kusinzia, matatizo ya kupumua na mkanganyiko wa kiakili. Dalili hizi zinaweza kuwa mbaya na mtu kupoteza fahamu katika kipindi cha saa 24-48.
- Hakuna chanjo ya ugonjwa huo kwa binadamu wala wanyama
(Chanzo: WHO, Vituo vya Udhibiti na Kinga dhidi ya Magonjwa)
Tags:
WADUDU NA MAGONJWA