KILA mwanamke hupitia hatua ya kupatwa na hedhi mara moja
kwa mwezi, ikiwa ni maumbile ya kawaida waliyoumbwa nayo. Lakini wanawake wengi
husumbuliwa na matatizo kadhaa siku chache kabla au wakati wa siku zao,
matatizo hayo hutofautiana kati ya mtu na mtu kutegemeana na afya ya muhusika.
DALILI ZA MATATIZO YA HEDHI
Siku chache kabla ya hedhi, baadhi ya wanawake hupatwa na
hofu na huwa wenye hasira. Husumbuliwa na mfadhaiko wa akili, huumwa na kichwa,
matiti hujaa maziwa, hukosa usingizi na kuvimba sehemu za siri. Hali hii
husababishwa na kukosekana kwa uwiano wa homoni (Homone imbalance) na hali hii
huweza kukoma ndani ya saa 24 baada ya kuanza hedhi.
MAUMIVU MAKALI YA HEDHI
Wengine hupatwa na maumivu makali sana wakati wa hedhi. Maumivu hayo huwapata
akina mama ama siku mbili ama tatu kabla au mara tu waanzapo siku zao. Hali hii
pia inasababishwa na kutokuwepo kwa uwiano wa homoni mwilini, ambako
kumesababishwa na ukosefu wa virutubisho fulani.
Wengine hutokwa na damu nyingi kuliko kawaida au kukaa
katika siku za hedhi kwa kipindi kirefu kuliko kawaida. Kuna sababu nyingi
zinazoweza kuchangia hali hii, ikiwemo kuugua kwa muda mrefu, kupatwa na hofu,
huzuni, mshtuko na sababu nyingine za kitabibu.
JUISI YA MBOGA ZIFUATAZO HUTIBU
Kwa kutumia vyakula asilia unaweza kuepukana na maumivu ya
mara kwa mara wakati wa siku zako. Katika orodha ndefu ya juisi za mboga
zinazotibu kwa uhakika matatizo yote ya hedhi, ni Kotimiri (Parsley), mboga ya
majani ambayo upatikanaji wake ni rahisi. Kwa mujibu wa watafiti, Kotimiri ina
uwezo wa kurekebisha uwiano wa homoni hivyo kuondoa matatizo kadhaa ya hedhi.
Inaelezwa kuwa uwezo wa Kotimiri kurekebisha matatizo ya
hedhi unatokana na kuwa na aina ya kirutubisho kiitwacho ‘Apiol’ ambacho pia
kimo miongoni mwa homoni za jinsia ya kike (estrogen). Maumivu na mvurugiko wa
siku hurejea katika hali ya kawaida kwa kunywa juisi ya Kotimiri mara kwa mara.
Aidha, juisi hiyo inapochanganywa na juisi ya viazi pori (Beet Root), karoti
au matango huwa na nguvu zaidi. Kiwango kinachoshauriwa kuchanganya kiwe na
ujazo sawa kwa kila aina ya juisi utakayochanganya. Juisi yenye mchanganyiko
huo ni rahisi kutengeneza na ni dawa inayoweza kumsaidia mwanamke wakati wote
wa maisha yake bila kuhitaji kutumia dawa zingine kali za kuzuia maumivu (pain
killers) ambazo huwa na madhara baadaye.
TANGAWIZI NAYO HUTIBU
Tangawizi nayo ni dawa nzuri sana ya kutibu matatizo yatokanayo na hedhi,
hasa katika tatizo la maumivu makali na kutokupata hedhi. Chukua kipande cha
tangawizi mbichi, kiponde na kiweke kwenye kikombe cha maji ya moto kwa dakika
chache, kisha tia sukari kiasi na unywe mchanganyiko huo, kwa siku mara mbili
kila baada ya mlo.
UFUTA NAO NI DAWA
Ufuta (Sesame) nao ni miongoni mwa mbegu za asili unazoweza
kula na kutibu matatizo ya hedhi. Saga ufuta na pata unga wake kisha uchanganye
na maji ya moto, kunywa mara mbili kwa siku. Kinywaji hiki huondoa maumivu
wakati wa hedhi kwa wasichana wadogo.
Ukitumia mara kwa mara kinywaji hiki cha ufuta, hutibu pia
tatizo la kupata hedhi kidogo. Pia unaweza kuchangaya maji ya kuoga ya
uvuguvugu na mbegu za ufuta zilizopondwa pondwa kiasi cha kiganja kimoja, nayo
hutoa nafuu kubwa kwa wanaosumbuliwa na maumivu, hasa ukitumia siku mbili kabla
ya siku zako.
PAPAI NALO NI DAWA
Mungu ametuumba na kutupa mazao mengi ambayo yana uwezo wa
kutatua matatizo yetu ya kiafya, iwapo tutagundua siri hiyo. Papai bichi nalo
linaelezwa na watafiti wetu kuwa lina uwezo wa kulainisha misuli ya njia ya
uzazi hivyo kufanya utokaji wa hedhi kuwa mwepesi usio na maumivu. Papai huwa
na manufaa zaidi kwa wasichana haswa kwa wale wenye tatizo la kutopata siku zao
kutokana na kuwa na ‘stress’ au mawazo. Utapata faida hiyo kwa kula mara kwa
mara tunda hilo
bichi (ambalo halijaiva lakini limekomaa)
Tags:
MAGONJWA YA WANAWAKE