Ugonjwa wa Kisukari tishio kwa watoto

WATALAAM wa ugonjwa wa kisukari hapa nchini wamesema asilimia 9.1 ya Watanzania wanaishi na ugonjwa huo kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2012.

Aidha, wataalam hao wamesema tatizo hilo pia likizidi kuwakumba watoto wadogo. 

Madaktari na wauguzi wamekutana jijini Dar es Salaam kujadili mbinu mbalimbali za kukabiliana na ugonjwa huo pamoja na kuwahudumia wagonjwa waliopatwa na tatizo hilo. 

Mratibu wa ugonjwa wa kisukari kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mariam Karomo, akizungumza na Nipashe alisema tatizo la ugonjwa huo kwa sasa linazidi kuwakumba watoto wadogo. 

Alisema watoto wadogo wanaokumbwa na ugonjwa huo hali hiyo inatokana na kurithi kutoka ukoo wao huku watu wazima akieleza kuwa ni kutokana na mtindo wa maisha wanaoishi. 

Mtalaam huyo alisema kisukari ni moja ya magonjwa hatari ambayo siyo ya kuambukizwa. 

Alisema vitu ambavyo huchangia ugonjwa huo ni unywaji pombe, uvutaji, sigara, kula vyakula vyenye mafuta, kutumia vinywaji vyenye sukari. 

Alisema ikiwa watu watatumia vitu hivyo katika maisha yao ya kila huku hawafanyi mazoezi ya mwili kuna uwezekano wa kukumbwa na ugonjwa wa kisukari. 

Kwa upande wake, mtalaam wa magonjwa ya kisukari kwa watoto kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dk. Edina Majaliwa, alisema kwa sasa hakuna takwimu sahihi za watoto wenye ugonjwa huo. 

Alisema jamii mara nyingi inaamini kwamba ugonjwa huo unawakumba watu wazima na kwamba imani hiyo inawafanya wazazi kutowapima watoto kubaini tatizo hilo. 

Alitaja dalili za ugonjwa huo kwa watoto wadogo kuwa ni pamoja na kukojoa kitandani mara nyingi wakati wa usiku, kupenda kula vitu vyenye sukari, kupenda kula pamoja na kupungua uzito. 

Watalaam hao wa afya walikutana jijini Dar es Salaam kwa siku tatu kujadili namna ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukizwa kikiwamo kisukari.

Post a Comment

Previous Post Next Post