Saratani (Cancer) ni ugonjwa unaotokana na seli za mwili zilizopoteza mfumo wake wa kugawanyika na hivyo hazipo katika hali yake ya kawaida. Seli hizo huweza kugawanyika bila mpangilio maalum na kuharibu mkusanyiko wa seli nyingine. Seli za saratani hutokea sehemu moja ya mwili na zinaweza kusambaa sehemu nyingine za mwili kupitia mfumo wa damu na limfu (lymph). Saratani inaweza kuwa ya kurithi au kusababishwa na hali ya mazingira ya vitu mbalimbali kama vile ulaji wa vyakula vyenye visababisha saratani (carcinogenic compounds), km. nyama iliyochomwa mpaka kuungua kidogo, ulaji usio bora, pombe, uvutaji sigara au mionzi hatari, aina ya madini kama “asbestos” na “lead”.
Zipo pia baadhi ya saratani zinazosababishwa na virusi kama vile saratani ya shingo ya kizazi. Saratani huweza kutokea kwenye sehemu mbalimbali za mwili kama vile mapafu, matiti, kibofu cha mkojo, shingo ya uzazi, ovari, utumbo, koo, mdomo, ngozi, n.k. Hali nzuri ya lishe na mtindo bora wa maisha ni kigezo muhimu sana katika kuzuia saratani na pia ni sehemu muhimu ya matibabu na kudumisha maisha bora baada ya matibabu ya saratani kumalizika. Matumizi ya baadhi ya vyakula huweza kuongeza uwezekano wa kupata baadhi ya saratani na vyakula vingine huweza kupunguza uwezekano wa kupata saratani. Uzito wa mwili unapozidi kiasi unaweza pia kuongeza uwezekano wa kupata baadhi ya saratani. Pamoja na mtindo bora wa maisha unaodumisha ulaji bora, mazoezi ya mwili na unyonyeshaji wa watoto wachanga, ni muhimu pia kupata na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya kuhusu upimaji unaoweza kugundua mapema baadhi ya saratani na kuzidhibiti. Mfano wa upimaji huo ni pamoja na upimaji wa matiti na shingo ya kizazi kwa wanawake. Kuhusu vipimo au uchunguzi unaohitajika, pata maelezo zaidi kutoka kwa wataalamu wa afya
Tags:
SARATANI(KANSA)
Lets see...
ReplyDelete