Hali nzuri ya lishe na mtindo bora wa maisha ni muhimu kwa kila binadamu, hivyo ni muhimu kila mtu apate taarifa za msingi za lishe bora. Hii ni pamoja na mtindo bora wa maisha ambao unazingatia kanuni bora za afya. Mtindo bora wa maisha ni pamoja na ulaji bora, mazoezi ya mwili, kuepuka matumizi ya pombe na tumbaku n.k. Mtindo bora wa maisha huuwezesha mwili kujikinga na maradhi mbalimbali hususan maradhi sugu na pia huboresha maisha kwa ujumla. Ulaji wa mlo kamili kila siku ni msingi wa afya bora. Mlo kamili Mlo kamili ni mlo ambao una mchanganyiko wa vyakula mbalimbali vyenye virutubishi vyote muhimu na vya kutosha ili kukidhi mahitaji ya mwili. Ili kudumisha hali nzuri ya lishe na afya bora kila mtu anahitajika kufanya yafuatayo: • Kula mlo kamili angalau mara tatu kwa siku ili kuuwezesha mwili kupata virutubishi muhimu na vya kutosha. • Kuhakikisha kuwa mlo kamili unakuwa na mchanganyiko wa vyakula kutoka makundi yote ya vyakula kama ifuatavyo: Vyakula vya nafaka (km. mahindi, ngano, mchele, ulezi, mtama na uwele), mizizi (km. viazi vitamu, viazi mviringo, magimbi, viazi vikuu, mihogo) na ndizi. Vyakula vya jamii ya kunde kama kunde, maharage, njugu mawe, mbaazi, njegere kavu, choroko, karanga, dengu na fiwi. Vyakula vya jamii ya wanyama: Nyama aina zote, samaki, maziwa, jibini, dagaa, mayai, wadudu wanaoliwa (km. kumbikumbi na senene). Lishe na Saratani 2 Vidokezo Muhimu Mboga-mboga: Aina zote za majani yanayoliwa (km. majani ya viazi/ matembele, majani ya kunde, maboga, mchicha, sukuma wiki, spinachi, kisamvu, mchunga, figili, mnafu, mlenda), mboga-mboga zingine kama karoti, bamia, nyanya, biringanya, maboga, zukini, matango, nyanya chungu, bitiruti. Matunda: Mapera, mabungo, ubuyu, ukwaju, nanasi, maembe, machungwa, malimau, ndimu, mafenesi, mastafeli, machenza, zambarau, topetope, pensheni, papai, mikoche, embe ng’ong’o,tikiti maji nk. Mafuta (km. yanayoganda au ya maji) na sukari (km. sukari nyeupe na guru) kwa kiasi. KUMBUKA: • Mchanganyiko wa vyakula mbalimbali uliwe pamoja kwa sababu vyakula/virutubishi hutegemeana katika kufanya kazi vizuri mwilini.
Tags:
SARATANI(KANSA)