Wafanyakazi watano wa Azam TV wafariki ajalini wakielekea Chato

aJALIHaki miliki ya pichaMCL
Watu saba wakiwemo wafayakazi watano wa Azam TV wamefariki katika ajali nchini Tanzania.
Ajali hiyo imetokea Shelui, Singida na kuhusisha magari mawili yaliyogongana uso kwa uso.
Wafanyakazi hao wa Azam TV walikuwa njiani kwenda kurusha matangazo mbashara ya uzinduzi wa Hifadhi ya Taifa ya Burigi-Chato.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida Sweetbert Njewike ameiambia BBC kuwa ajali hiyo imetokea saa mbili asubuhi hii leo.
Wafanyakzi wa Azam walikuwa wanasafiri kwenye basi aina ya Coaster wakitokea Dar es Salaam.
Gari lao liligongana uso kwa uso na lori ambalo lilikuwa likitokea Mwanza.
Wafanyakazi wa Azam TV waliofariki kwenye ajali hiyo ni Salim Mhando (muongozaji wa matangazo), Florence Ndibalema (Mhandisi wa Sauti), Sylvanus Kasongo (Mhandisi Mitambo) na wapiga picha wawili Said Haji na Charles Wandwi.
Watu wengine wawili waliofariki ni dereva wa gari ambalo Azam TV walilikodi pamoja na msaidizi wake, majina ya wawili hao bado hayajapatikana.
Wafanyakazi watatu wa Azam TV wamejeruhiwa ambao ni Artus Masawe, Mohammed Mwinshehe na Mohammed Mainde.
Mtendaji Mkuu wa Azam Media Tido Mhando amesema majeruhi wawili wapo katika hali ya mahututi na mmoja hali yake inaendelea vizuri.
Kwa mujibu wa Tido, maiti zipo hospitali ya Iramba mkoani Singida, na majeruhi wapo Hospitali ya Igunga mkoani Tabora.
"...utaratibu wa kupata helikopta za kusafirisha miili ya marehemu na majeruhi kuja hospitalini Muhimbili jijini Dar es Salaam inaendelea," amesema Tido kupitia runinga za Azam Media Ltd.

Rais Magufuli atuma salamu za pole

Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa Kampuni za Said Salim Bakhresa kufuatia vifo hivyo.
"Nimeshtushwa na vifo hivi, nampa pole Mwenyekiti Ndg. Said Salim Bakhresa, ndugu wa Marehemu wote, Mtendaji Mkuu Ndugu Tido Mhando na wafanyakazi wote wa Azam Media Ltd, waandishi wa habari na wote walioguswa na msiba huu," taarifa ya Ikulu imemnukuu rais Magufuli akisema.
Naye Waziri wa Utalii Hamisi Kigwangala ameomboleza vifo hivyo akisema moyo wake unatokwa machozi ya damu.

Post a Comment

Previous Post Next Post