Shirika la kupima viwango vya ubora wa bidhaa nchini Uganda The Uganda National Bureau of Standards (UNBS) linatarajiwa kufanya utafiti na vipimo zaidi kuhusu ubora wa kinywaji cha Natural Power SX , kinywaji cha kuongeza nguvu mwilini kinachodaiwa kuwa na dawa ya Viagra .
Kulingana na gazeti la The Sunday Monitor nchini Uganda vipimo vya maabara vilivyofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti matumizi ya dawa nchini Uganda NDA ,vilibaini kwamba kinywaji cha Natural Power SX kina Sildenafil Citrate, ambayo hukuzwa kama Viagra.
The Sunday Monitor linasema kuwa, NDA mnamo mwezi Disemba 28 kupitia barua iliotiwa saini na bwana David Nahamya kwa niaba ya katibu wa mamlaka hiyo bi Dona Kusemererwa, liliripoti kwa Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la ubora wa bidhaa nchini Uganda Dkt. Ben Manyindo kwamba mlalamishi alidai kwamba baada ya kutumia kinywaji hicho nguvu zake za kiume ziliongezeka kwa muda mrefu mbali na kiwango cha mipigo ya moyo pamoja na kutokwa na jasho kusiko kwa kawaida.
Kufuatia malalamishi hayo mamlaka ilichukua sampuli ya bidhaa hiyo na kuichunguza.
Kwa mujibu wa gazeti hilo matokeo yake yalionyesha kuwa bidhaa hiyo ya Slidenafil Citrate iliwekwa katika kinywaji hicho kulingana na barua hiyo .
Slidenafil , inayouzwa kwa jina maarufu kama Viagra ni dawa inayotumika kutibu matatizo ya nguvu za kiume pamoja na tatizo la shinikizo la damu. Hutumika kwa kula ama kudungwa moja kwa moja katika mishipa ya damu
Kwa mujibu wa gazeti la The Sunday Monitor kisa hicho kinajiri wakati ambapo mamlaka ya NDA inayosimamia dawa nchini Uganda mwezi uliopita ilionya kwamba dawa ya Viagra ilipatikana imechanganywa katika dawa za miti shamba.
Vyombo vya habari vilinukuu mamlaka ya NDA ikisema kwamba asilimia 55.08 ya dawa za mitishamba pamoja na dawa za vyakula tofauti zimechanganywa na Sldenafil pamoja na dawa nyengine hatari.
Swala hilo liliwasilishwa kwa shirika la ubora wa bidhaa na mamlaka ya kudhibiti utumizi wa dawa ambao wanasema kuwa walipata sampuli za Natural Power SX ambazo zilikuwa zimetiwa dawa ya Viagra baada ya kupokea malalamishi kutoka kwa mteja aliyekuwa na wasiwasi.
Watengenezaji
Kinywaji hicho hutengezwa nchini Zambia.
Kwa mujibu wa gazeti la the Sunday Monitor, Mlalamishi kulingana na NDA alikabiliwa na ongezeko la nguvu za kiume kwa takriban saa sita mbali na mipigo ya moyo isio ya kawaida baada ya kunywa kinywaji hicho.
Bwana Godwin Muhwezi mkuu wa idara ya uhusiano mwema aliambia gazeti la Jumapili la The Monitor kwamba kundi la wataalam watachunguza madai ya barua hiyo kutoka NDA na kutoa mipango ya kupima bidhaa hiyo zaidi.
''Nitafanya majadiliano zaidi kabla ya kuthibitisha kwenu ni hatua gani tutakayochukua. lakini kile ambacho tutahitajika kufanya ni kuchunguza yaliomo katika barua ili nkwenda kuchukua vipimo kwa uchunguzi zaidi'', alisema.