Ugonjwa wa kisukari(diabetes) kwa mtoto, utautambuaje?

Ulimwengu unapoadhimisha siku ya ugonjwa wa kisukari, utafiti uliyofanywa na shirikisho la kimataifa la ugonjwa wa kisukari (IDF) umebaini kuwa wanne kati ya wazazi watano hawana uwezo kung'amua dalili za mapema za ugonjwa huo kwa watoto wao.
Awali ugonjwa wa kisukari ulihusishwa na watu wanene na wazee lakini miaka ya hivi karibuni watoto wachanga pia wamejikuta wakikabiliwa na maradhi hayo.
Ili kufahamu kwanini watoto pia wanakabiliwa na ugonjwa huu BBC imezungumza na Farhia Mohammed kutoka mtaa wa Eastleigh jijini Nairobi, anayemuuguza mtoto wake wa miaka minane ambaye alipatikana na ugojwa wa kisukari akiwa mdogo.
Farhia anasema hana budi kumpikia chakula maalum mwanawe ili aweze kudhibiti kiwango cha sukari mwilini mwake.
''Nikiamka nafikiria kile kitu nitampatia, lazima iwe chakula asili, kama anaenda shule lazima apate mlo kamili''
Mtoto huyo aligunduliwa kuwa anaugua kisukari alipokuwa na miaka minne. Mama Farhia anasema hakuwa na ufahamu mwanawe anaugua kisukari
''Niliona mtoto anaenda msalani mara kwa mara hali ambayo nilihisi si ya kawaida''
Anasema alipompeleka hospitali hawakuruhusiwa kurudi nyumbani kwa sababu mtoto alihitajika kupewa matibabu ya dharura.
Vipimo vya sukari mwiliniHaki miliki ya pichaREUTERS
Lakini swali ni je ni kwanini watoto wanapatikana na maradhi ya kisukari wakiwa wadogo?
Abdisalan Mohammed ambaye ni daktari wa watoto anasema ugonjwa wa kisukari umekuwepo tangu zamani.
Anaongeza kuwa tofauti na miaka ya nyuma siku hizi kuna maabara ambayo wataalamu wanatumia kufanya utafiti ili kubaini ikiwa mtoto anaugua ugonjwa huo.
Dkt Abdisalan anasema''kwa kweli 10% ya ugonjwa wa kisukari unapatikana kwa watoto wachanga kwa hivyo watu wasifikirie kuwa huu ni ugonjwa wa watu wazima pekee''
Watoto hususan hupatikana na aina ya kwanza ya kisukari ambayo inahitaji mgonjwa kudungwa dawa ya insulin ili kudhibiti kiwango cha sukari mwilini.

Kisukari ni ugonjwa gani?

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2017 ya shirikisho la kimataifa la ugonjwa wa kisukari karibu watu milioni 15.5 waliyo na umri kati ya miaka 20-79 wanaishi na ugonjwa huo barani Afrika.
Ugonjwa wa kisukari hutokea pale kongosho (pancrease) inaposhindwa kutengeneza homoni au kichocheo aina ya Insulin, au pale mwili unaposhindwa kutumia vizuri kichocheo hicho.
Hali hiyo husababisha ongezeko la kiwango cha sukari kwenye damu (hyperglycemia).
Kazi ya Insulin ni kuondoa glucosei katika damu na kuingiza katika misuli, seli za mafuta na ini, ambako hutumiwa kama nishati.
Dkt Abdisalan anasema kuwa chakula kinapoyeyushwa matukio kadhaa hutokea ikiwa ni pamoja na sukari inayoitwa glucose ambayo ni chanzo cha nguvu mwilini kuingia katika damu.
Mwanamke akijipima uzaniHaki miliki ya pichaGETTY IMAGES
Tukio la pili hutokea katika kiungo kinachoitwa kongosho (pancrease) ambacho hutengeneza kichocheo cha Insulin.
Kazi ya Insulin ni kuondoa glucosei katika damu na kuingiza katika misuli, seli za mafuta na ini, ambako hutumiwa kama nishati.

Kuna aina mbili kuu ya ugunjwa wa kisukari,

Aina ya kwanza ya kisukari
Mtu hupatikana na aina hii ya kisukari ikiwa seli maalumu zinazotengeneza homoni ya insulin zinapokosekana katika tezi kongosho.
Pia kongosho zinapoharibika kutokana na sababu yeyote ile husababisha ukosefu kabisa au upungufu wa kichocheo hicho kwenye damu.
Kwa mujibu wa wataalamu wa matibabu aina hii ya kisukari ni hatari sana.
Huwaathiri zaidi watoto na vijana
Aina ya pili ya kisukari
Katika aina hii ya kisukari, insulin huzalishwa kwa kiwango cha kutosha isipokuwa tatizo lipo kwenye ufanisi na utendaji kazi wake.
Upungufu wa mazoezi ni hatari kwa afya ya mwanadamuHaki miliki ya pichaEMPICS
Image captionUpungufu wa mazoezi ni hatari kwa afya ya mwanadamu
Mara nyingi mtu hupatikana na aina hii kisukari ukubwani.
Hii inatokana na kupungua kwa utendaji kazi wa homoni ya insulin, au seli kushindwa kutumia insulin ipasavyo.
Hali hii mara nyingi husababishwa na unene uliopitiliza, au hali ya kutofanya mazoezi kabisa.
DALILI ZA UGONJWA WA KISUKARI
  • Kukojoa mara kwa mara
  • Kuhisi kiu kali na kunywa maji kwa kiwango cha kupitiliza (polydipsia).
  • Kuhisi njaa na kula mara kwa mara (polyphagia).
  • Kuchoka haraka
  • Kupungua uzito
  • Vipele mwilini
  • Kutoa harufu ya acetone inayofanana na harufu ya pombe.
  • kuhisi maumivu ya tumbo na kupoteza fahamu
Mtu anayeugua kisukari huwa na kiwango cha juu vya sukari kwenye damu kwa sababu mwili wake hauwezi kupeleka sukari kwenye seli za mafuta, ini na misuli ili ihifadhiwe kwa ajili ya kuzalisha nguvu.
Hali hali ya kuwa na kiwango cha juu cha sukari kwenye damu huenda ikaharibu moyo, macho, miguu na figo
Hata hivyo tiba maalum na uangalizi mzuri kwa watu wanaougua kisukari inaweza kuwahakikishia maisha marefu yenye afya.

Post a Comment

Previous Post Next Post