Utakaso, ni utamaduni muhimu sana kwa kabila la wakara kaskazini magharibi mwa Tanzania, ambapo mwanaume au mwanamke anapofiwa na mwenzake analazimika kutafuta mtu wa kushiriki naye tendo la ndoa baada tu ya mazishi ili kuondokana na mikosi mbalimbali kabla ya kuanza kuchangamana na jamii.
Utamaduni huu umekuwa ukitekelezwa kwa kasi baada ya ajali ya MV NYERERE iliyotokea Miezi kadhaa iliopita katika kisiwa hicho na kuua mamia ya watu.
Utamuduni huu ni wa kawaida kwa pande zote mbili, yani mwanamke na mwanaume pale pindi tu watakapofiwa na wake ama waume zao, na hufanyika siku nne baada ya kuzika.
Mwanamke au mwanamme aliyefiwa anatakiwa kufanya tendo la ndoa na mtu atakayechaguliwa na ndugu zake ili aweze kuonekana msafi tena na kuchangamana na jamii.
Utamaduni huu umekuwa kwa miaka mingi katika jamii ya Wakara ambapo wengi hufanya hivyo kutokana na msukumo wanaupata kutoka kwa jamii hususani wazazi na wazee wa kimila.
Kwa mujibu wa wazee wa kimila usipofanya utaratibu huo baada ya kufiwa na mweza wako basi matatizo yatakupata wewe na familia yako ikiwemo watoto.
Salome lusatu alifiwa na mume wake katika ajali ya mv nyerere, siku nne baada ya mazishi alilazimika kutakaswa, alitafutiwa mtu na kisha akafanya naye tendo la ndoa, baada ya hapo akaendela na maisha yake kama kawaida.
''nilitafutiwa mwanaume kisha tukatakasana, ilikua siku nne baada ya msiba na sikuweza kukataa waliniambia kuwa watoto wangu watakufa kifo kibaya na wataumwa matumbo, na ugonjwa mwingine, sasa ikabidi tuu nifanye huu utamaduni sikua na namna nyingine hata kama sitaki'' anasema salome.
Utamaduni huu unaweza kufanyika pia kwa mume na mke waliofiwa na wenza wao wakafanya tendo la ndoa kama njia ya kutakasana.
Emanuel Marwa alifiwa na mkewe na katika sehemu ya kukamilisha utamaduni huo akalazimika kufanya tendo la ndoa na mwanamke aliyefiwa na mumewe hivyo wakawa wote wawili wamekamilisha utamaduni.
''walinitafutia, shemeji yangu alinitafutia mwanamke mwenye matatizo kama yangu, tukalala wote baada ya hapo ikawa nimemaliza utamaduni'' anasema Marwa.
Marwa ameongeza pia alikua na wasiwasi lakini hakuwa na namna kwasababu angetukanwa na kusemwa sana na wazee wake wa kimila.
Utamaduni huu una maana gani?
Kwa jamii ya wakara, hii ni sehemu muhimu ya kutekeleza urithi wa utamaduni ulioachwa na wazee wa kimila.
Ukifanya utamaduni huu ina maana umekua msafi tena baada kufiwa lakini pia unaanza maisha mapya katika jamii.
Na usipofanya utamaduni huu, basi huwezi hata kutembelea nyumba za jirani zako kwani wewe unakua si msafi.
Lakini mbali na kuwa watu wengi wa jamii ya ukara wanafanya utamuduni huu na kuufuata, Baadhi ya watu wachache sana hawataki kusikia kutokana na kuwa waumini wa dini za kikisto hivyo utamaduni kama huo kwao ni dhambi.
Wazee wa kimila wanasema kuwa sasa hivi mambo yamebadilika hivyo hata utekelezaji wa utamaduni si kama zamani.
'' zamani kulikua na mtakasaji anaitwa OMWESYA ,maalum wa kufanya hii kazi, lakini sasa tunaweza kukuruhusu ukachagua mwenyewe mtu wa kukutakasa kisha ukaenda mkatakasana'' anasema mzee Damian.
Utathibitisha vipi mtu ametakasika?
Tendo la ndoa hufanywa kwa siri baina ya wale wanaoshiriki, katika utamaduni huu wakati tendo inafanyika watu wa makamo ya wanaoshiriki tendo hilo , pamoja na wazee wa kimila husubiri kwa maeneo ya karibu na chumba ambapo tendo linafanyika, baada ya kukamilika wanaojitakasa hutoka nje na kusema wamefanikiwa ama la hawajafanikiwa.
Ikiwa wamefanikiwa basi wanakuwa wametakasika na anaweza kuendelea na maisha na kujichanganya katika jamii kama kawaida.
Utamaduni huu umeelezwa kuwa unaweza kuwa sehemu ya kuchangia maambukizi ya virusi vya ukimwi, kwani hakuna matumizi ya kinga wala kupima afya kabla ya kufanya Tendo hilo.
Katika sehemu ya kuondoa tamaduni kama hizi zinazoleta madhara katika jamii, Wizara ya Afya nchini Tanzania imekua na kampeni mbalimbali katika meoeneo ya Ukara ili kuleta uelewa kwa jamii.
''uzuri ni kwamba elimu inatolewa na maafisa kutoka wizara ya Afya hadi katika ngazi ya Kata, tatizo ni kubwa hivyo inachukua muda ili kuweza kuondoa kabisa tamaduni kama hizi, si jambo la siku moja'' anasema Mwanaisha Moyo afisa ustawi kutoka wizara ya Afya.
Utamudi huu umekuwepo kwa miaka mingi, na baadhi ya wakazi wa Ukara hawaoni kama kuna haja yoyote ya Kuachana na mila hizi. Na wazazi pamoja na Wazee wa Kimila wamekua na mchango mkubwa katika kuendeleza na kuwalazimisha vijana kufuata na kufanya Utakaso.
Tags:
UZAZI