Afya ya umma nchini Uingereza imewashauri watu walio na zaidi ya miaka 30 kujipima mitandaoni ili wapate kuelewa umri wa mioyo yao, hatua inayowasaidia kufahamu iwapo wako kwenye hatari ya kupatwa na mshutuko wa moyo au kiharusi.
Mfumo huo unatambua kuwa asilimia 80 ya mishtuko wa moyo na kiharusi kwenye watu walio chini ya miaka 75, inaweza kuzuiwa ikiwa afya ya moyo itaboreshwa.
David Green mwenye miaka 59 alifanyiwa uchunguzi.
"Wakati mbaya zaidi ni wakati niliambiwa kwa moyo wangu ulikuwa wa miaka kumi zaidi ya umri wangu na kuwa amaisha yangu kuishi duniani yalifupishwa," aliiambia BBC.
"Kwa uhakika ilinichukua muda kukubali lakini nikaamua kuchukua hatua na kufanya kitu kuweza kuirekebisha hali hiyo."
Hakuwa amesikia lolote kuhusu umri wa moyo.
"Nina miaka 59 kwa hivyo nilifikiri kuwa labda ingekuwa na miaka 62 au 63, kwa hivyo miaka 10 zaidi ni kitu kilinishangaza sana.
"Waliniambia nifanye kitu la sivyo sitaweza kufurahia malipo yangu ya uzeeni'.
"Nafikiri hicho ndicho kilikuwa kitu muhimu kwangu.
Unene wa ju wa mwili, lishe duni, kukosa kufanya mazoezi pamoja na mpigo wawa juu ya moyo ni kati ya mambo hatari kwa moyo yanayoweza kubadilishwa.
Jinsi ya kuboresha afya ya moyo wako:
- Wachana na uvutaji sigara
- Fanya mazoezi
- Dhibiti uzito wako
- Kula chakula chenye kiwango cha juu cha ufumwele
- Punguza mafuta
- Kula mboga na matunda kila siku.
- Punguza kiwango cha chumvi
- Kula samaki
- Punguza pombe
Karibu watu milioni mbili wamepima miaka ya mioyo yao na asilimia 78 ya washiriki wana mioyo yenye umri wa juu kuliko umrit wao wenyewe.
Zaidi ya watu 84,000 hufariki kutokana na mshutuko wa moyo na kiharufi kila mwaka nchini Uingereza.
Mfumo huo wa kupima unauliza maswali 16 rahisi ya mitindo ya maisha na kutoa makadirio ya umri na kutabiri uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo au kiharusi kwenye umri fulani.
Pia unatoa mawaidha kuhusu mambo yanayohusu kubadili mitindo ya maisha kuwasaidia watu kupunguza umri wa mioyo yao.