Muungano wa Wanafamasia nchini Kenya unakadiria kwamba 30% ya dawa nchini ni ghushi.
Hilo limejitokeza hususan kwa dawa za kupambana na ugonjwa wa Malaria aina ya antibiotiki zilizoonekana kuathirika pakubwa.
Biashara ya dawa ghushi duniani inakisiwa kufikia dola bilioni 30 kulingana na shirika la afya Duniani WHO.
Mwandishi wa kitengo cha afya cha BBC Life Clinic ameweza kuchunguza jinsi dawa duni huingizwa nchini Kenya na uwezo wa kusababisha madhara
Hatari kwa maisha ya Wakenya
Dolphine Anyango anaishi katika kitongoji duni cha Kibera, jijini Nairobi, alinunua dawa katika duka moja la dawa kujitibu
Nyumbani kwake tulimpata akifuma shanga, biashara anayojishughulisha nayo kujikimu kimaisha.
Dolphine alipokuwa akichambua shanga mezani, niliona kovu karibu na jicho lake. Nilitaka kufahamu zaidi
"Niliamka asubuhi nikajikuta jicho limeanza kufura, nikaenda dukani nikanunua dawa, lakini jicho liliendelea kufura zaidi kuliko lilivyokuwa awali kumaanisha dawa haikufanya kazi.
'Ni umaskini unaotufanya tusiweze kwenda kwenye hospitali kubwa, kwahivyo tunanunua tu za hapa katika kijiji na tunasema bora uhai'.
Dawa duni huingizwa nchini Kenya mara nyingi kupitia bandari au viwanja nya ndege, na kumekuwa na juhudi za hivi karibuni ambazo zimefanikisha vita dhidi ya dawa ghushi.
Ibrahim Bulle ni afisa wa shirika la kukabiliana na bidhaa bandia
"Hivi karibuni shirika la kupambana na dawa ghushi lilifanikiwa kuzuia dawa ghushi za kupanga uzazi kutoka China na zilifichwa katika kontena la mizigo.
Takriban tembe 31,000 zilikuwemo ndani - hizo zina thamani ya $60,000 "
Swala muhimu ni je, serikali inashugulukia vilivyo kukandamiza biashara hii ya dawa duni?
Nilirejea Kibera na kuzungumza na mwanafamasia kuhusu hoja hii na akaniambia kwamba, maafisa kutoka shirika la kukabiliana na dawa bandia nchini Kenya wanatumia mamlaka visivyo hasa maeneo ambayo asilimia kubwa ya maduka ya dawa hayajasajiliwa.
"Hawa maafisa wa bodi ya dawa na sumu wanapokukamata, wanakunyanyasa na kutaka uwalipe Kshs 50,000. Ndio sababu kila wanaopkuja wamiliki maduka ya dawa Kibera huyafunga na kutoroka. Wanapokupelekea kituo cha polisi wanakunyanyasa na kutaka utoe hongo. Ndiyo sababu kila mtu hutoroka''.
Niliziwasilisha shutuma hizi kwa Dr James Nyikal, mwenyekiti wa kamati ya afya bungeni.
"Bila shaka kuna swala la rushwa - kuna maafisa waliofichuliwa ambao wamekuwa wakisambaza dawa ambazo hazijakaguliwa. Halijakufa, kwahiyo maafisa hao bado wapo wanaendelea."
Kwa upande wao, shirika la kukabiliana na dawa Bandia, Pharmacy and Poisons Board nchini Kenya, linakiri kwamba shida ipo.
Christabel Khaembani afisa katika bodi hiyo.
'Najua tatizo lipo lakini naamini jitihada zaidi zinahitajika ili kuweza kupata makadirio kamili ya ukubwa wa tatizo'.
Tulipom'bana kwa maswali makali zaidi, kwamba yeye kama kiongozi anafanya nini?
Alisusia kulijibu swali kwa kueleza kwamba maswali yetu tunastahili kuyaelekeza kwa usimamizi wa bodi hiyo.
Tulijaribu kutafuta majibu zaidi kutoka kwenye bodi hiyo kupitia njia tofuati ikiwemo barua pepe lakini hatukufaulu na hadi pale tutakaposhuhudua mabadiliko, Wakenya, kama Dolphine watazidi kuhatarisha maisha yao.