Pombe
Siyo siri kuwa pombe husababisha matatizo makuwa ya kiafya, yakiwemo magonjwa ya moyo, ini pamoja na majeraha yatokanayo na ajali zitokanazo na ulevi. Ni dhahiri kuwa vinywaji halisi vilivyotengenezwa kwa matunda bila kilevi ni bora zaidi kwa afya yako kuliko vile vyenye kilevi.
Licha ya kuwepo kwa kampeni kadha wa kadha zinazopinga matumizi ya pombe, bado watu wengi wameendelea kushikilia kinywaji hiki bila kufahamu athari zake kwenye afya zao. Fuatilia hapa chini athari 12 za pombe kiafya.
1. Matatizo ya moyo
Unywaji mkubwa wa pombe husababisha matatizo mbalimbali ya moyo kama vile cardiomyopathy, ambapo mishipa ya moyo hudhoofika na kushindwa kusukuma damu. Jambo hili huweza kusababisha damu kuganda na kusababisha kiharusi (stroke). Pombe huchangia sana katika kudhoofisha mishipa ya moyo hivyo kupelekea ugonjwa huu wa cardiomyopathy na mengine hatari.
2. Tatizo la ini
Unywaji wa pombe unaweza kusababisha maradhi ya ini yajulikanayo kama Cirrhosis; ambayo ni maradhi ya ini kushindwa kufanya kazi yake kutokana na uharibifu wa muda mrefu. Uharibifu huu husababisha seli za ini kuwa makovu na kushindwa kufaya kazi vyema. Utafiti umebaini kuwa pombe huchangia sana katika kuharibu seli hizi za ini.
3. Shinikizo la damu
Unywaji wa pombe hasa kupitiliza umedhibitishwa kuchangia kwa kiasi kikubwa maradhi ya shinikizo la damu. Imebainikia kuwa pombe huathiri mfumo wa usukumaji wa damu mwilini jambo ambalo hupelekea shinikizo la damu na baadye matatizo mengine kama kushindwa kwa figo, ini n.k.
4. Magonjwa ambukizi
Mara nyingi mtu anapokunywa pombe hupoteza uwezo wa kutawala mwili na maamuzi yake. Hivyo ni rahisi baada ya mtu kunywa pombe akafanya au akajiingiza kwenye matendo hatarishi yanayoweza kumfanya kuambukizwa magonjwa kama vile UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa.
5. Ugonjwa wa anemia
Anemia ni ugonjwa unaotokana na kushindwa kwa seli nyekundu za damu kusafirisha oksijeni ya kutosha kwenda kwenye mwili. Hivyo unywaji wa pombe hupunguza uwezo wa seli nyekundu za damu kusafirisha oksijeni ya kutosha hivyo kupelekea ugonjwa wa anemia.
6. Saratani
Utafiti uliofanywa na daktari Jurgen Rehm, PhD, wa chuo cha Toronto umebaini kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kupata saratani kutokana na unywaji wa pombe. Utafiti huu ulieleza kuwa tatizo huanza pale ambapo mwili hubadili kilevi (alcohol) kuwa kemikali iitwayo “acetaldehyde”.
Saratani huweza kutokea kwenye koo, shingo, mdomo na mapafu. Pia aliongeza kuwa atari inaongezeka pale ambapo mtumiaji wa pombe pia ni mvutaji wa sigara.
7. Kusinyaa kwa ubongo
Kadri umri wa mtu unavyozidi ndivyo na ubongo wake unavyozidi kusinyaa. Hivyo unywaji wa pombe huharakisha kusinyaa kwa ubongo kwa silimia 1.9. Hili hupelekea matatizo yatokanayo na kusinyaa kwa ubongo kama vile kupoteza au kupungua kwa uwezo wa kumbukumbu.
8. Msongo wa mawazo
Pombe huathiri mchakato wa kikemikali wa ubongo (Kemia ya ubongo). Kutokana na utafiti uliofanywa, imebainika kuwa watu wanaokunywa pombe nyingi hukabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo. Msongo wa mawazo ni chanzo cha maradhi mbalimbali kama vile shinikizo la damu, matatizo ya akili, matatizo ya moyo na wakati mwingine kifo.
9. Maumivu ya miguu (gout/jongo)
Gout au jongo ni ugonjwa wa miguu unaotokana na kukusanyika kwa asidi kwenye viungio vya mifupa. Mara nyingi ugonjwa huu hujitokeza sana majira ya baridi. Pamoja na vyanzo vya sababu za kurithi za ugonjwa huu, pombe imedhihirika kuchangia kwa kiasi kikubwa kutokea kwa ugonjwa huu.
10. Uharibifu wa mfumo wa fahamu
Hivi leo pombe mbalimbali hutengenezwa kwa kutumia kemikali mbalimbali, kemikali hizi kwa kiasi kikubwa huwa na athari kwenye mfumo wa fahamu. Pombe huathiri mifumo na utendeji kazi wa mfumo mzima wa fahamu na kusababisha matatizo kama vile udhaifu wa misuli na matatizo katika milango la fahamu.
Hii ndiyo sababu mtu anayekunywa pombe kali anashindwa kuhisi landa za vitu kama vile chumvi au pilipili vyema; hivyo hujikuta akitumia kwa kiasi kikubwa.
11. Kusinyaa kwa uso na macho
Unywaji mkubwa wa pombe husababisha kusinyaa kwa uso na macho hasa kwa wale wanaokunywa usiku. Mara ngingi uwatazamapo wanywaji wakubwa wa pombe utaona hata sura zao zimebadilika na kuonekana zimezeeka au kuchoka kuliko awali.
Ni dhahiri umewahi kumwona kijana mlevi wa miaka 25 lakini anaonekana kama mzee wa mika 40. Hii ni kutokana na athari zinazosababishwa na unywaji mkubwa wa pombe.
12. Huathiri mifumo ya uzazi
Kumekuwa na mawazo kadha wa kadha kuhusu pombe na maswala ya uzazi. Wengine huamini kuwa pombe huboresha maswala ya uzazi huku wengine wakiamini kuwa pombe huathiri maswala ya uzazi. Ukweli ni kuwa pombe ina madhara kadha wa kadha kwenye maswala ya uzazi kama ifuatavyo:
Husababisha kukutana kimwili kusiko salama.
Huathiri nguvu za kiume.
Huathiri mtoto aliye tumboni kwa mama.
Husababisha watu kufanya matendo binafsi au ya aibu hadharani.
#FAHAMU HILI