Magonjwa (STI's)
Magonjwa yakuambukizana kupitia kufanya ngono - Haya kwa kimombo yanaitwa STI au Sexually Transmitted Infections.
Kufanya ngono iliyosalama
Ukweli. Aambukizo mengine ya magonjwa ya sehemu za siri, kama vile uvimbe mgumu, hutokea kwa sababu nyingine mbali na kufanya mapenzi. Kwa mfano, mara nyengine kama umetumia dawa ya kupambana na viini ya aina ya bacteria, antibiotics au dawa za kumeza za kuzuia mimba.
Ukweli. Kuambukizwa magonwja ya zinaa hakumaanishi una wapenzi wengi.
Ukweli. Mengi ya magonwja ya zinaa yanaweza kutibiwa kwa dawa za kupambana na viini yaani anti-biotics
Ukweli. Yakiachwa bila kutibiwa, baadhi ya magonjwa hayo yanaweza kusababisha madhara ya kudumu kwa afya yako na wakati mwengine hata kukusababishia ugumba au utasa.
Ukweli. Unaweza kupata ugonjwa wa zinaa hata unapokuwa katika hedhi.
Ukweli. Afrika ndiyo kanda ambayo imeathiriwa vibaya zaidi na janga la ukimwi kote duniani.
Mambukizo hutokea pale maji maji ya mwili kama vile mate, damu, manii majimaji ya ukeni nk – ya mtu ambae tayari ameambukizwa, yatatangamana na ya mtu ambae hajaambukizwa. Hii mara nyingi hufanyika wakati wa ngono ya kuingiliana kimwili, au ya kunyonyana sehemu za siri.
Baadhi ya majonjwa hayo (lakini sio yote) yanatibika, lakini yasipotibiwa yanaweza kusababisha madhara ya kudumu. Kumbuka maambukizi ya ukimwi na virusi vya HIV pia mara nyingi hufanyika kupitia kufanya ngono.
Na kumbuka pia bado hakuna tiba ya Ukimwi, wala chanjo dhidi ya virusi vya HIV.
Kwa sasa hivi kinga bora dhidi ya magonjwa ya zinaa, ni kutofanya ngono kabisa au kutumia kondom kwa kufuata maagizo kikamilifu, na kufanya ngono iliyosalama
Nitajua vipi kama nimeambukizwa magonjwa yanayoathiri afya ya uzazi?
Wanawake:
Maji maji au ute unaotoka kwenye uke ni sawa kabisa, lakini wanawake wanapaswa kutafuta usaidizi wa kimatibabu wakigundua lolote kati ya yafuatayo:-
Majimaji ya ukeni ambayo yana harufu isiyo ya kawaida na yenye rangi tofauti na wingi kuliko ilivyo kawaida.
Maumivu au kusikia kama unachomeka au mwasho wakati wa kwenda haja ndogo.
Maumivu na mwasho katika maeneo ya uke.
Maumivu ya ukeni wakati wa kufanya ngono.
Vidonda na malengelenge katika eneo la uke.
Kumbuka, baadhi ya maambukizi huenda yasiwe na dalili. Hii haimaanishi kwamba huwezi kumwambukiza mpenzi wako, au kwamba hayawezi kukudhuru kiafya. Kama una wasi wasi, ni vyema kuchunguzwa na daktari haraka iwezekanavyo, ama katika kliniki.
Wanaume:
Mwanaume anapaswa kuenda kutafuta ushauri wa daktari kama atajipata na dalili zifuatazo:
Majimaji kutoka uumeni ambayo yana harufu isiyo ya kawaida, au yakiwa mengi.
Kuhisi mwasho ndani ya uume, wakati na baada tu ya kwenda haja ndogo
Vijidonda na sugu ama malengelenge juu au katika sehemu za kiume.
Vipele au uvimbe katika sehemu za siri.
Kwa mara nyingine tena, kumbuka maambukizo mengine kama ya virusi vya ukimwi yanaweza kuwemo mwilini kimya kimya kwa mda bila dalili zozote kujitokeza. Unaweza kuwa hutaona dalili yoyote kwanza, lakini haimaanishi kwamba huwezi kuwaambukiza wengine.
Kama umefanya mapenzi bila kutumia kinga na una wasi wasi huenda umeambukizwa, nenda ukafanyiwe uchunguzi na daktari.
Magonjwa ya kawaida yanayoambukiza sehemu za siri (viungo vya uzazi)
Cystitis– Huu ni uvimbe mgumu
Huambukiza kupitia bacteria ambazo huishi chini ya ngozi, eneo la sehemu za siri na hata kwenye utumbo mkubwa.
Dalili: Dalili kubwa ni maumivu makali wakati wa haja ndogo, na kujisikia kutaka kwenda chooni mara kwa mara. Maumivu hayo yanaweza kuendelea kuwa makali kwa haraka sana.
Huwakumba zaidi wanawake hasa wakati wa hedhi na wakati wa hali fulani nyenginezo kama vile kuwa na uja uzito, au kuugua ugonjwa wa sukari.
Usipotibiwa kwa haraka unaweza kusambaa hadi kwenye figo na kusababisha madhara mabaya zaidi.
Matibabu: Kunywa maji kwa wingi au vinywaji majimaji kama maji ya matunda (juisi hasa ile ya cranberry yafaa zaidi!) Unapoona tu dalili za kwanza kwanza, juisi hiyo inaweza kusaidia sana. Hata hivyo ni vyema kumuona daktari kwa uchunguzi na atakupendekezea dawa zinazokufaa.
Thrush: Huu ni ugonjwa wa kuvimba vimba ndani kwa ndani mwilini. Kwa kawaida husababishwa na 'fungus'- kukua kupita kiasi kwa kitu kama hamira. Ugonjwa huu unaweza kusambazwa kwa njia ya ngono lakini pia unaweza kutokea kutokana na sababu nyingine, kwa mfano kama kuvaa chupi, suruali iliyokubana zaidi, au kama unaugua ugonjwa wa sukari. Ugonjwa huu unaweza kuwapata wanawake kwa wanaume.
Dalili: Dalili kubwa kwa wanawake, ni kupata maumivu na kujikuna kwenye mashavu ya upenyo wa uke na sehemu ya kupitishia haja kubwa (mkunduni). Yaani kujihisi mfano wa kuanza vidonda katika eneo la sehemu za siri. Hali hiyo huandamana na kutokwa na majimaji mazito meupe kutoka ukeni yenye harufu kama hamira. Sehemu hizo huenda zikawa nyekundu zaidi, wanaumenao, huenda wakahisi mwasho kwenye uume, hasa nchani … (kichwa cha mboo) na kuhisi kama karaha ya kupata vidonda. Pia wakati mwingine uume hutokwa na majimaji au ute mzito wa njano .
Matibabu: Pindi ukigunduliwa ugonjwa wa Thrust hutibika kwa usahisi. Daktari hupendekeza vidonge au krimu maalum ambazo zinapatikana kwa wingi, kwenye maduka ya madawa.
Trichomonas vaginalis – kwa kifupi (TV)- Hiki nacho ni kijidudu cha bacteria, kidogo kinachoambukiza kupitia ukeni na kwenye mrija wa kupitishia mkojo.
Dalili: Dalili za ugonjwa huu ni vigumu kuzigundua … hasa kwa wanaume. Dalili kwa mwanamke aliyeambukizwa ni kutokwa na majimji au ute wa rangi ya kijani – manjano hivi, ambao huenda ukawa na harufu kama ya samaki.
Matibabu: Ugonjwa huu unaweza kutibiwa kwa urahisi, kwa madawa maalam ya kupambana na viini antibiotics. Ili kuepuka kuambukizwa upya, na kusambaa zaidi kwa ugonjwa huu inabidi mpenzio pia nae atibiwe.
Magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya ngono
Magonjwa yanayoambukizwa kupitia ngono ni baadhi ya maambukizi yanayotokea mara kwa mara kote ulimwenguni, na huwaathiri watu wa kila rika na asili, wanawake kwa wanaume.
Bora tu wewe hufanya ngono, iwe ya baina ya mke na mume, au iwe baina ya wasenge au wasagaji, ama kushiriki katika aina iwayo ya ngono, basi ni vyema kuchukua tahadhari.
Njia moja ni kutumia vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi haya. Kwa mfano kutumia kondom na mpenzio, kila mara mnapofanya ngono, hadi pale nyote wawili mtakapokuwa mna hakika kabisa kwamba hakuna uwezekano wowote wa ninyi wawili kuambukizana magonjwa ya ngono.
Hebu tuangalie orodha hii ya baadhi ya mengine yakuambukuzana kupitia ngono.
Chlamydia - Husababishwa na viini vya bacteria na waweza kuathiri uke, mrija wa kupitisha mkojo, uume au sehemu ya kupitishia haja kubwa.
Dalili: Kwa wanawake dalili hazionekani kwa urahisi. Ubaya ni kuwa ugonjwa huo unaweza kuathiri fallopian tubes – yaani mirija ya kupitia mayai kutoka kwa ovari hadi kwenye nyumba ya uzazi hivyo basi kusababisha utasa. Wakati mwengine dalili hii unaweza kuiona - kutokwa na majimaji ya ukeni yasiyo ya kawaida na kuhisi maumivu wakati wa kukojoa.
Kwa wanaume ugonjwa huu huathiri mrija wa kupitishia mkojo, uzuri ni kwamba dalili huonekana wazi, kama vile uume kutokwa na ute na kusikia maumivu wakati wa kukojoa.
Matibabu: Ni pamoja na kufanyiwa uchunguzi wa mkojo au damu. Unapotambuliwa daktari hupendekzeza dawa maalum ya kumeza. Kama umefanya mapenzi hivi karibuni basi yafaa mpenzi huyo aarifiwe ili nae atibiwe pia.
Kisonono (Gonorrhoea)
Huu husababishwa pia na bacteria. Unapofanya mapenzi na mtu mwenye kisonono unaweza kuaathiri viungo kama vile uke, uume, sehemu ya haja kubwa na ya haja ndogo, na hata koo au mdomo kama ukifanya mapenzi ya kunyonyana.
kisonono bacteria
kisonono bacteria
Dalili: Wanawake hutokwa na ute mwingi wa njano au kijani kutoka ukeni na kusikia maumivu wakati wa kukojoa. Kwa wanaume uume uliathirika hutoa ute wa njano au kijani, na kupata maumivu wakati wa kukojoa.
Pia kuna uwezekano wa kuwashwa ama kutokwa na maji maji katika sehemu ya kupitishia haja kubwa. Ingawa hivyo baadhi ya watu hawaoni dalili zozote kabisa lakini bado wanaweza kuwambukiza wanaofanya mapenzi nao.
Matibabu: Iwapo matibabu hayatapatikana kwa haraka kuna hatari ya mirija ya kupitisha mayai (fallopian tubes) kuharibika na hivyo kusababisha utasa.
Kama una kisonono usifanye tena mapenzi hadi utakapofanyiwa uchunguzi na kupewa madawa ya kutibu ugonjwa. Ni muhimu sana kumfahamisha mpenzio ili nae pia atibiwe.
Herpes Huu husababishwa na aina fulani ya kirusi, kama kile kinachosababisha mafua na vidonda vya mdomoni. Mbali na kusambazwa kupitia ngono pia husambazwa kupitia kufanya mapenzi ya kunyonyana sehemu za siri.
Dalili: Ni Kupata vidonda ukeni au uumeni mfano wa vile vinavyotokea mdomoni wakati wa homa kali ya mafua.
Matibabu: Sasa kuna dawa na krimu za kupambana na virusi hivi. Lakini kumbuka hata unapotibiwa virusi vya herpes bado hubaki mwilini mwako na vinaweza kuzusha tena vindonda. Pia kama umja mzito unaweza kumwambukiza mtoto wako, hivyo basi kama una vijidonda ni vyema kumjulisha mkunga wako ama daktari ili upate matibabu yafaayo.
Magonjwa mengine yanayoathiri njia ya mkojo (Non Specific Urethritis kwa kifupi NSU)
NSU ni herufi zinazotumiwa kuelezea magonjwa ya bacteria yanayoathiri mfereji wa kupitisha mkojo yaani urethra. Magonjwa hayo husambazwa kwa kupitia kufanya mapenzi.
Dalili: Kwa wanaume dalili kubwa ni kutokwa na ute, kutoka kwenye tundu ya uume na huenda akahisi maumivu wakati wa kukojoa. Huenda ukasikia maumivu au kuwashwa-washwa.
Matibabu: Majimaji yakitoka kwenye uume, isipokuwa mkojo au manii, ni lazima uchunguzwe na daktari, au nesi katika kliniki ya afya ya uzazi. Unaweza kutibiwa kwa kutumia vidonge vya anti-biotics.
Kaswende (Syphilis)
Ugonjwa huu nao husababishwa na bacteria Treponema Pallidum
Dalili zake hazionekani kwa urahisi. Huenda ukaanza kwa kijidonda au kipele kwenye uke au uume au sehemu ya kupitishia haja kubwa. Kidonda hiki kinapopona usidhani ndio mwisho wa maambukizo la! Viini hivyo vinaweza kubaki mwilini kimya kimya kwa miaka mingi!
Matibabu: Ni bora daktari kufanya uchunguzi wa damu kwani majimaji ya ukeni au uumeni huenda uchunguzi wake usionyeshe viini vya kaswende. Kaswende ni hatari, kama haitibiwi, inaweza kusababisha utasa au ugumba, na hata kuathiri moyo, mishipa ya damu, ngozi ya mwili, mifupa na hata ubongo na kurukwa na akili.
Hata hivyo matibabu yake ni rahisi – Zipo dawa aina (antibiotics) zinazoweza kutibu kaswende kabisa. Ili kuzuia kuenea kwa maradhi hayo ni vyema mpenzio nae pia atibiwe.
Tags:
MAGONJWA YA ZINAA