"Nilikuwa namlaumu Mungu mbona ameniacha nikawa bado hai, angeniua," ni tamko linaloashiria kizungumkuti ambacho Darlan Rukih alikumbana nacho maishani.
Binadamu huwa wa jinsia mbili, kike na kiume, na karibu kila shughuli katika jamii huelezwa kwa kufuata jinsia hizi mbili.
Lakini Rukih alizaliwa akiwa na viungo vya jinsia zote mbili kwa pamoja - huntha.
Akiwa na umri mdogo, alidhalilishwa na kubaguliwa, na kumfanya karibu akate tamaa maishani.
"Hii ilikuwa shida kati yangu na watoto wenzangu kwa sababu hawakuwa wananiona kama nafanana nao. Walijaribu sana kunitenga. Nikienda kwa wasichana wananifukuza niende kwa waume, nikienda kwa wanaume wananifukuza niende kwa wasichana," aliambia mwandishi wa BBC Anne Soy.
"Hakuna aliyetaka kujihusisha nami. Wakati mwingine ningetembea nikipitia vichakani, nikiogopa kwamba watu wangeniona. Baadhi walinishambulia. Kunao waliotaka kunivua nguo waone maumbile yangu.
"Nilikuwa kama kitu cha kuudhi, iliniuma sana.
"Mimi nilijiona kwamba mimi si mtu muhimu kabisa katika hii dunia ambapo mimi nastahili tu kifo".
Katika kipindi hiki kigumu, alikuwa anayaelekeza maswali yake kwa muumba, Mungu. Mbona akamuumba akiwa hivyo?
"Nilikuwa nasema ningekuwa Mungu au niwepo wakati naumbwa, ningemwambia Mungu badala ya kuniumba binadamu ungeniumba hata mnyama kwa sababu mnayama hawe akambagua mnayama mwenziwe."
Mamilioni ya watoto huzaliwa wakiwa na viungo vya kike na kiume kwa pamoja duniani, na hutatizika kutangamana na wengine katika jamii.
Katika jamii nyingi za Afrika, watoto kama hao walikuwa wakiuawa punde wanapozaliwa.
Darlan alibahatika kwamba mamake aliamua kumlinda tangu utotoni.
"Nilikuwa natembea naye kila mahali. Akienda shuleni na pia sikumruhusu aende ziwani kuoga hadharani na wenzake kwenye ziwa. Nilimwandalia eneo maalum nyumbani ambapo angetumia kama bafu kuoga," mamake anasema.
Darlan anasema alipojitambua alipata tayari mamake amemtambulisha kwa ulimwengu kama mvulana.
Kwa kuwa tayari alikuwa amelelewa kama mvulana, Darlan na mamake waliamua kufanya lolote wawezalo kusitiri usichana wake.
"Sikuwa na mtu wa kunisikiliza, isipokuwa mamangu. Kwa sababu mamangu alikuwa mtu mfuata dini, alikuwa ananipa moyo na kuniambia kwamba ni Mungu aliyeniumba hivyo, kwamba halikuwa kosa, hivyo mimi sikuwa matunda ya makosa," anasema Darlan.
Matatizo kwa Darlan yalijitokeza tena pale alipoanza kubalehe.
Alikuwa muda wote ameamini kwamba alikuwa mvulana lakini mwili wake na viungo vyake vilianza kubadilika. Aidha, alianza kupata hedhi.
Ni hapo ambapo mamake alimpeleka hospitalini na baada ya kupimwa na daktari akafahamishwa kwamba alikuwa na viungo vya uzazi mara mbili.
'Viungo vya kike ndani yako vina nguvu kuliko vya kiume," aliambiwa na daktari.
Darlan hata hivyo alitaka kuendelea kuwa mvulana.
Mamake alijitolea kumsaidia katika hilo na alimtafutia homoni za kupunguza nguvu za kike.
Sio wakati huo tu ambapo mamake alikuwa amemuwezesha kuendelea kuishi.
Katika jamii yao ya Waluo, watoto huntha waliuawa punde walipozalia.
Turorabwon ndilo jina la kitendo hicho cha kuogofya.
Wakunga katika jamii yake Darlan walikuwa wakiwaua watoto huntha muda mfupi baada yao kuzaliwa.
"Walikuwa wanawaua. Iwapo mtoto huntha angezaliwa, moja kwa moja alitazamwa kama laana na hakuruhusiwa kuishi. Mkunga alitakiwa kumuua na kumwambia mamake mtoto kwamba mtoto alizaliwa akiwa amefariki," anasema Seline Okiki, ambaye ni mwenyekiti wa kundi la wakunga kutoka magharibi mwa Kenya kwa jina Ten Beloved Sisters.
Katika kutekeleza Turorabwon, wakunga wangesema kwamba walikuwa „wamevunja kiazi kitamu".
"Hii ilikuwa na maana kwamba walitumia kiazi kitamu kuvunja fuvu la kichwa cha mtoto huyo," anasema Anjeline Naloh, katibu wa kundi hilo.
"Wazazi hawakuwa na usemi kuhusu hilo. Ilikuwa kwamba mtoto kama huyo hata hakufaa kuishi muda wa kutosha kuanza kulia."
Siku hizi sheria za nchi zimewazuia wakunga kufanya hivyo na pia wanawake wengi wanajifungulia hospitalini.
Madamu mamake alimficha, Darlan alinusurika kifo.
Sasa, ana umri wa miaka 42 na kutokana na kipaji chake cha uimbaji, amejulikana sana magharibi mwa Kenya.
Anasimamia pia kituo cha watoto mayatima ambao amewapa makao.
Na mamake bado humsaidia maishani.
"Nimefurahi kwa sababu Mungu amemwezesha kunawiri. Naye anawasaidia watu wengi. Ningeshawishika kumuua nani angewasaidia watu hawa?" anasema mamake.
Darlan sasa anapaza sauti yake kuwatetea huntha wenzake. Anaitaka serikali kuwatambua watu wenye maumbile kama yake, kuhakikisha maslahi yao yamezingatiwa na sheria kutungwa ili kuhakikisha haki zao za kibinadamu zinaheshimiwa.
Ingawa hakuna takwimu halisi kuhusu idadi ya Wakenya ambao ni huntha, madaktari wanaamini iwapo kiwango hiki ni sawa katika nchi nyingine, basi wanaweza kuwa 1.7%.
"Ningependa serikali iwape nafasi watu wenye jinsia ya tatu, kwa sababu natambua na nakubali kwamba kuna wanaume na wanawake duniani na tena, kuna wato wenye jinsia ya tatu na huntha. Kwa hivyo, wanafaa kutambuliwa kwa jinsia yao kwenye katiba, kwa sababu wapo kwenye jamii," anasema Darlan
Tags:
TAARIFA ZA KIAFYA