Hospitali kadhaa nchini Tanzania zimefungwa kwa kutozingatia masharti na vigezo vya kiusalama vilivyowekwa na serikali.
Maafisa wanasema hospitali 102 zimefungiwa leseni nchini humo kwa makosa ya kutoa huduma za afya huku wakitumia mashine mbovu na kutumia watu ambao hawana ujuzi.
Swali ni je ni hatua gani inaweza kuchukuliwa kuhimiza matumizi salama ya sayansi nyuklia?
Ili kujibu swali hilo na masuala mengine, wajumbe kutoka mataifa 46 barani Afrika wanahudhuria mkutano wa kimataifa wa uratibu wa miradi ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia, mjini Arusha kaskazini mwa Tanzania,
''Ukiongelea nyuklia, watu wengi wanafikiria unaongelea mabomu'' anasema Profesa Lazaro Busagala, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Atomiki nchini Tanzania.
Anasema neno nyuklia limetokana na chembe chembe ambazo zimeutengeneza ulimwengu au zimetengeneza vitu mbali mbali.
Prof.Busagala ameongezea kuwa teknolojia hiyo ni salama ikitumiwa vizuri.
''Teknolojia ya nyukilia inaweza kuwa na madhara makubwa kwa binadamu kama haitatumiwa kwa usahihi',' alisema.
Kinachojadiliwa katika mkutano huo wa Arusha ni kuangalia mambo mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta ya afya, kilimo, lishe, maji, mazingira na sekta nyingine nyingi namna ambavyo zinaweza kutumia teknolojia ya nguvu za nyuklia.
Matumizi ya teknolojia ya nyukilia
- Teknolojia ya nishati ya nyuklia ina uwezo wa kuzalisha umeme kwa viwango vikubwa.
- Takriban asilimia 15 ya umeme wote unaotengenezwa duniani unatokana na nishati ya nyuklia.
- Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA,Teknolojia ya nyuklia inaweza kutumiwa kama vile X Ray inavyotumiwa kupiga picha ili mtu aweze kujulikana ameumia wapi.
- Pia inaweza kutumiwa kugeuza kidogo chembe chembe za uhai ya wanyama ama ya mimea ilikuwasaidia wanasayansi kujua matatizo inayokabili wanyama au mimea.
- Teknolojia hiyo inatumika kuzalisha mimea ambayo inastahamili vitu kama wadudu na magonjwa
Nishati ya nyuklia hatahivyo ina matatizo na hatari ambazo ni pamoja na ajali na mnururisho hatari.
Tatizo ambalo halijatatuliwa ni suala la kutunza kwa njia salama takataka nururifu hatari zinazobaki baadaye kwa muda wa miaka elfu kadhaa.
Wakati wa ufunguzi rasmi wa mkutano huo Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Tekenolojia William Ole Nasha alisema kuwa serikali ya Tanzania kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imefanikiwa kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya Teknolojia ya Nyuklia.
Bwana Ole Nasha amesema Shirika hilo linafadhili miradi mingi katika sekta mbali mbali hnchini ikiwemo sekta ya afya ambapo imewezesha kupatikana kwa vifaa mbali mbali vya uchunguzi wa tiba na maradhi ya saratani ambavyo vimefungwa katika hospitali ya Rufaa ya kanda ya ziwa Bugando jijini Mwanza na Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kiufundi ya IAEA barani Afrika, Profesa Shaukat Abdulrazak amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha matumizi salama ya teknolojia ya nyukilia kwenye sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya, kilimo, mifugo, maji, viwanda na ujenzi.
Mwishoni mwa mwaka jana, Kenya iliomba msaada wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kuisaidia kuimarisha matibabu ya saratani katika hospitali mbili kubwa nchini humo na pia kueneza huduma hizo za matibabu katika miji mingine mitatu.
Waziri wa Nishati wa Kenya alihutubia kikao cha mawaziri cha IAEA mjini Vienna Austria na kufichua kuwa, nchi hiyo ya Afrika Mashariki iko mbioni kuunda kiwanda cha kuzalisha nishati ya nyuklia kwa ajili ya kuimarisha huduma za matibabu.