Madaktari nchini Saudi Arabia wamesema wamefanikiwa kuwatenganisha wasichana wawili pacha waliozaliwa wakiwa wameungana eneo la Gaza.
Wasichana hao kwa jina Farah na Haneen walifanyiwa upasuaji katika hospitali ya watoto ya Mfalme Abdullah.
Walikuwa wanatumia mguu mmoja kwa pamoja lakini kila mmoja ana moyo wake na mapafu yake.
Wasichana hao walisafirishwa hadi Saudi Arabia pamoja na baba yao baada ya madaktari kuonya kwamba maisha yao yangekuwa hatarini iwapo wangesalia katika Ukanda wa Gaza.
Watoto hao walizaliwa Oktoba wakiwa wameshikana kwenye tumbo na sehemu ya chini ya mwili.
Madaktari walitangaza kwamba upasuaji huo ulifanikiwa kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na shirika la habari la Saudi Arabia.
Shirika hilo lilisema upasuaji huo ulihusisha kutenganisha utumbo wao, ini na nyonga, na ulifanywa kwa hatua tisa.
Pacha hao walisafirishwa Saudi Arabia Desemba kwa matibabu hayo, baada ya kusafirishwa kutoka Gaza hadi Jordan.
Upasuaji huo haungewezekana Gaza, ambapo Umoja wa Mataifa unasema viwango vya huduma ya afya vimeshuka kutokana na kuendelezwa kwa marufuku ya kutoingiza bidhaa ukanda huo, ambayo inatekelezwa na Israel na Misri, mizozo ya kivita, migawanyiko ya kisiasa miongoni mwa Wapalestina na kupunguzwa kwa bajeti.